Mwanasiasa mkongwe, Dk Wilbroad Slaa (76) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka la kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa X (zamani twitter).
Dk Slaa alifikishwa mahakamani hapo jana jioni, Januari 10, 2025 akikabiliwa na kesi ya jinai namba 993 ya mwaka 2025.
Dk Slaa aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden, alisomewa shtaka na Wakili wa Serikali, Clemence Kato anayeshirikiana na mawakili Tumaini Mafuru na Abdul Bundala.
Wakili Kato, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki alidai mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 9, 2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikielezwa kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa X katika akaunti ya Maria Sarungi aliandika ujumbe uliosomeka:
"Wakubwa wametafutana, nikisema wakubwa namaanisha Mwamba na Samia, na wala hatuna maneno ya kumung'unya... na kimsingi wamekubaliana Suluhu Samia amekubali atatoa pesa, Suluhu Samia amekubali ataongeza nguvu ya pesa ni dhahiri atatoa pesa... hizo ni hela za Watanzania wanazichezea Samia na watu wake."
Awali Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lilithibitisha kumshikilia mwanasiasa mkongwe, Dk. Willibrod Slaa, kwa mahojiano.
Taarifa hiyo ya polisi ilitolewa baada ya kusambaa taarifa kuwa alikamatwa juzi akiwa anafanya mazoezi karibu na nyumbani kwake, Mbweni mkoani Dar es Salaam.
Aidha, ilisambazwa sauti inayoelezwa kuwa ni ya Dk. Slaa akieleza kuwa amekamatwa na Jeshi la Polisi na anapelekwa Kituo cha Polisi cha Mbweni.
"Nawajulisha tu kwamba kuna polisi wamenifuata, nitawajulisha kitakachotokea, napelekwa Mbweni kituoni," Dk. Slaa alieleza.
Akizungumza na Kituo cha Redio cha Wasafi FM jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro, alisema ni kweli wanamshikilia Dk.Slaa kwa mahojiano.
Alisema wakati wanaendelea kuhoji wataangalia maelekezo ya mifumo ya kisheria kisha hatua zingine zitafuata.
"Ni sahihi daktari yupo, tuko naye na tumekuwa na mahojiano naye kwa baadhi ya mambo na mahojiano yetu yanakwenda vizuri. Kwa hiyo tunaangalia mifumo ya kisheria inatuelekeza nini cha kufanya. Naamini taarifa zaidi zitatolewa baadaye," alisema Kamanda Muliro.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED