WANANCHI 14,624 waliopimwa magonjwa ya macho katika kipindi cha mwaka 2024 mkoani Shinyanga, wamebainika kuwa na matatizo makubwa ya ugonjwa wa macho, wengi wakiwa na mtoto wa jicho.
Hayo yalibainishwa juzi na Mratibu wa Huduma za Macho mkoani Shinyanga, Dk. Joseph Edward, alipozungumza na waandishi wa habari kutokana na utolewaji wa matibabu bure ya macho kwa wananchi mkoani hapa kutoka kwa madaktari bingwa wa macho wa Hospitali ya Dr Agarwals tawi la Mwanza.
Dk. Edward alisema takwimu hizo ni za miezi 10 iliyopita na kuwa kati ya wananchi hao 14,624 waliokutwa na matatizo hayo huku 1,213 wakiwa na tatizo la mtoto wa jicho na kwamba waliwafanyia upasuaji.
“Ujio huu wa madaktari bingwa wa macho hapa mkoani Shinyanga, utasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua matatizo ya macho kwa wananchi wa mkoa huo, ambalo linawasumbua sana,” alisema.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, Dk. Moshi Lyoba, alisema wananchi wengi wamejitokeza kupata matibabu hayo na kwamba kwa asubuhi tu ya jana waliandikisha wananchi zaidi ya 250, na kuonyesha kwamba tatizo la macho ni kubwa.
Daktari Bingwa wa Macho, Abubakari Mwatute, kutoka Hospitali ya Macho Dr. Agarwals Tawi la Mwanza, alisema kati ya wananchi 10 ambao wanawafanyia uchunguzi, saba hadi wanane wanakabiliwa na tatizo la mtoto wa jicho.
Mmoja wa wananchi waliopatiwa matibabu hayo, John Lucas, aliiomba serikali kuendelea kushirikiana na wadau wa afya na kuwapeleka madaktari bingwa wa macho ili wasaidiwe kupata matibabu bure.
Alisema asilimia kubwa wanashindwa kupata huduma hiyo kutokana na kutokuwa na uwezo wa kifedha kuwafuata katika hospitali za kibingwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED