MKURUGENZI Mtendaji na Daktari Bingwa wa Hospitali ya Shree Hindu Mandal Dar es Salaam, Dk. Kaushik Ramaiya, amepata Tuzo ya Heshima ya Pravasi Bharatiya Samman 2025 (PBSA) kutoka kwa Rais wa India.
Tuzo hiyo imetokana na mchango wake wa kipekee wa kutoa huduma ya matibabu kwa jamii.
Tuzo hiyo ilitolewa jana katika Mkutano wa 18 wa Pravasi Bharatiya Diwas uliofanyika Bhubaneswar, Odisha unaolenga kusherehekea mchango wa diaspora wa India katika nchi wanazoishi.
Kwa mujibu wa taarifa, tuzo ya PBSA ni ya heshima ya juu zaidi inayotolewa na serikali ya India kwa watu wa nchi hiyo, watu wenye asili ya India au mashirika yanayoendeshwa na watu wa India kutambua mafanikio yao makubwa ndani na nje ya nchi.
Dk. Kaushik, raia wa Tanzania mwenye asili ya India, amekuwa akifanya utafiti kwa miaka mingi kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, yakiwamo uhimilivu wa sukari mwilini na hatari za magonjwa ya moyo hasa miongoni mwa jamii za Wahindi barani Afrika.
Mtaalamu huyo wa magonjwa ya ndani (Endocrinologist) pia anafanya kazi na watoto wenye ugonjwa wa kisukari aina ya kwanza, kisukari cha ujauzito, dalili za kimetaboliki na matatizo ya moyo yanayotokana na matumizi ya dawa za kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI.
Pia anashirikiana na Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutekeleza programu za kisukari na magonjwa yasiyoambukiza katika hospitali za kanda, mikoa, wilaya na vituo vya afya Tanzania.
Dk. Kaushik amechapisha zaidi ya makala 100 katika majarida ya kitaaluma na hivi karibuni alichaguliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Dk. Kaushik ni raia wa nne wa Tanzania mwenye asili ya India kupokea tuzo hiyo. Wengine ni Jayantilal Keshavji Chande (2005), Dk. Rajni Kanabar (2010) na Hajiat Shamim Parkar Khan (2019).
India ni nchi inayotoa diaspora wengi zaidi duniani na ni hazina muhimu kwa taifa. Diaspora wa India wamekuwa wakikuza uhusiano wa kitamaduni na kuimarisha ushawishi wa India duniani kwa kutangaza utamaduni, urithi, mila, na vyakula vyake.
Pia wanachangia kuleta maendeleo ya nchi wanazokaa na kuimarisha mahusiano ya pande mbili. Ili kuheshimu mchango wa diaspora ya India, Serikali ya India imekuwa ikiadhimisha Pravasi Bharatiya Divas kila Januari 9 tangu mwaka 2003.
Mkutano wa Pravasi Bharatiya Divas hufanyika kila baada ya miaka miwili kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya jamii ya Wahindi waishio nje ya India na serikali ya India, huku ukiwapa fursa ya kuungana na mizizi yao ya kitamaduni.
Mwaka huu, Mkutano wa 18 wa Pravasi Bharatiya Divas ulifanyika Bhubaneswar, Odisha kuanzia Januari 8 hadi 10, 2025, ukiwa na kaulimbiu "Mchango wa Diaspora kwa Bharat Ilioendelea.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED