Mbowe: CHADEMA itakuwa imara zaidi

By Restuta James , Nipashe
Published at 08:58 AM Jan 11 2025
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.
Picha:Mtandao
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amekoleza joto la uchaguzi ndani ya chama hicho kwa kusema mgombea atakayeshindwa na kuamua kuhama, atakiacha kikiwa imara.

Mbowe ambaye anatetea nafasi yake ndani ya CHADEMA, anachuana na Makamu wake (Bara), Tundu Lissu, kwenye uchaguzi uliopangwa kufanyika Januari 21, mwaka huu.

Akihojiwa jana na kituo kimoja cha redio mkoani Dar es Salaam. Mbowe alisema chama hicho ni taasisi kubwa kuliko kiongozi na mgombea yeyote na kwamba madai ya mgombea kushindwa kwenye uchaguzi na ‘kusepa na kijiji’, hayana nguvu ya kukipasua.

“CHADEMA ni kubwa kuliko Lissu. Ni  kubwa kuliko Mbowe. Hiki chama kimebeba matumaini ya mamilioni ya Watanzania wanaotumaini kitaleta mabadiliko katika nchi hii. Kila mmoja ana wafuasi kwa nafasi yake. Nguvu  ya kila mmoja ndani ya CHADEMA inatokana na umoja wetu.

“Yeyote anayefikiri atasepa na kijiji kama wanavyosema vijana wa mjini, atachoka sana. Yeyote anayefikiri akiondoka CHADEMA itameguka… sikiliza, kuna watu 300 hapa Dar es Salaam wanaomba nafasi za uongozi. Kuna watu wanasema CHADEMA itakufa kama TLP na NCCR-Mageuzi. Hivyo  vyama vilikuwa bado vichanga mno ndiyo maana walioondoka walivipasua,” alisema.

Mbowe alisema chama hicho kimeweka mizizi nchini nzima kwenye mabaraza yake ya Vijana (BAVICHA), Wanawake (BAWACHA) na 
 Wazee (BAZECHA) na kina wanachama kuanzia ngazi ya vijiji.

“Tuna mamilioni ya wapigakura. Tumejijenga na hiki chama ni taasisi. Chama cha kidemokrasia kilichojengwa kama CHADEMA hakiwezi kudhoofishwa na mtu mmoja. Siamini kwamba kuna mtu akitoka CHADEMA chama kitapasuka. Siamini kama wanachama wa CHADEMA wapo kwa sababu ya sura zetu sisi viongozi. Naamini wapo kwa sababu ya malengo ya pamoja ambayo tumeamua kuyapigania,” alisema.

Alisema hana ugomvi na Lissu wala mgombea yeyote ndani ya CHADEMA na minyukano inayoendelea inamsikitisha.

“Lissu nina historia ndefu naye. Ninakaa  namwangalia Lissu ambaye nimekaa naye, nimefanya naye kazi, nimeshirikiana naye kifamilia, kisheria, kisiasa, kibunge, halafu anatoa kauli dhidi yangu, kweli kibinadamu hainipendezi. Najipa uvumilivu sana kuvumilia jambo hili. 

“Namwomba sana Mungu anisaidie nisijenge chuki na kisasi juu ya haya kwa sababu yanapita; nafunga sana, naomba Mungu atuvushe salama, lakini zaidi ya yote, nisibaki na chuki na mtu,” alisema na kuongeza kuwa kitendo cha viongozi wakuu kugombea nafasi ya uenyekiti kinatafsiri kwamba mafahali wawili hawakai zizi moja.

Alisema hata yeye (Mbowe) akishindwa kwa haki haitakuwa shida kwake kwa kuwa anaamini katika mchakato wa kidemokrasia ambao chama hicho kimeujenga. Alisema ikiwa atashinda, ataendelea kufanyakazi na Lissu pamoja na wanachama wengine.

“Si Lissu tu na wengine wengi walioshindwa katika ngazi mbalimbali tunawahitaji, tunahitajiana pamoja na tofauti zetu. Pamoja  na mapungufu yetu bado tunahitajiana,” alisema.

Alisema wanaosema ‘Mbowe must go’ wanapaswa kutambua kwamba chama hicho kinahitaji hadi walio nje na kwamba kuna maisha baada ya Januari 21. Alisema dhana ya uongozi wa kisiasa inakwenda na malengo ya pamoja kama mchezo wa mpira wa miguu unaohitaji nguvu ya pamoja na kushinda.

Mbowe alisema CHADEMA imefika kuwa taasisi imara kwa kujengwa na Watanzania wengi wakiwamo wasio wanachama na kwamba minyukano inayoendelea ndani ya chama hicho ni kutokana na ukubwa na mafanikio kilichopata kwa muda mrefu.

MABADILIKO YA KATIBA

Kuhusu mabadiliko ya katiba ya chama hicho kuweka ukomo wa uongozi, alisema ni mchakato unaoweza kuchukua muda mrefu kwa kuwa baada ya kupita ngazi mbalimbali, inafikishwa kwenye mkutano mkuu ambao hufanyika mara moja katika kipindi cha miaka mitano.

Mabadiliko ya katiba ya CHADEMA ni moja ya agenda ya Lissu ambaye amesema akiingia madarakani ataifumua na kuisuka upya ili pamoja na mambo mengine, kuweka ukomo wa uongozi.

Kuhusu kumtuma Mwenyekiti wa Kanda ya Victoria, Ezekiel Wenje, Mbowe alisema ni uzushi na propaganda kumhusisha na mgombea yeyote kwa kuwa kila mwanachama mwenye sifa ana haki ya kugombea uongozi.

KAMATI KUU

Baada ya mahojiano na Clouds Media, Mbowe alihudhuria kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA, ambacho kilikuwa kinaongozwa na Lissu kwa muda.

Baadhi ya wajumbe waliohudhuria kikao hicho ni John Heche anachuana na Wenje kwenye nafasi ya Makamu Mwenyekiti (Bara), ambaye anamuunga mkono Lissu.

Lissu na Mbowe kama kawaida, jana walikaa pamoja wakati wa kikao hicho, kilichofanyika makao makuu ya CHADEMA, Mikocheni mkoani Dar es Salaam.