Mabilioni Korea kukuza uchumi Tanzania

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:43 AM Jan 11 2025
Mabilioni Korea kukuza uchumi Tanzania.
Picha:Mtandao
Mabilioni Korea kukuza uchumi Tanzania.

WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema Dola za Marekani bilioni 2.5 zilizoahidiwa na Korea Kusini kwa Tanzania hivi karibuni, zitasaidia kutekeleza miradi muhimu ya maendeleo itakayochangia kusisimua ukuaji wa uchumi wa nchi na maisha ya Watanzania kwa ujumla.

Dk. Nchemba alisema hayo juzi alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania, Eunju Ahn. Pamoja  na mambo mengine, walijadili namna ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizo mbili. 

“Nchi yetu inasubiri kwa hamu kubwa utekelezaji wa miradi inayotokana na fedha hizo na hata katika hotuba yake ya mwisho wa mwaka 2024, Rais Samia Suluhu Hassan,  alielezea kwa kina fedha hizo zitakavyotumika kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali yenye lengo la kutimiza ajenda ya kitaifa ya kuwaletea Watanzania maendeleo,” alisema.  

 Dk. Nchemba alisema makubaliano ya miradi itakayotumia fedha hizo iko katika sekta muhimu za maendeleo itakayochangia kukuza ajira, uchumi na maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA). 

Waziri Nchemba aliahidi kuwa Tanzania iko tayari kuongeza kasi ya ushirikiano kati ya nchi hizo ili kufanikisha malengo ya uhusiano uliodumu kwa miaka mingi kati yake na Korea kwa faida ya wananchi wa pande hizo mbili. 

Balozi Ahn kwa upande wake alisema Korea inaitazama Tanzania kama mdau wake mkubwa wa maendeleo na haijawahi kushuhudiwa nchi yoyote Afrika ikipewa fedha nyingi kiasi cha dola za Marekani bilioni 2.5 kwa wakati mmoja kama ilivyofanyika kwa Tanzania. 

Ahn alisema kupitia fedha hizo, Korea itaisaidia Tanzania kutekeleza miradi 12 ya kimkakati iliyowasilishwa na serikali, ambayo inatarajiwa kukuza uchumi wa nchi kupitia miradi mbalimbali itakayotekelezwa na serikali na sekta binafsi. 

Alisema Korea inaiona Tanzania kuwa nchi yenye maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii na kwamba muda mfupi ujao itafikia viwango vya juu vya ukuaji wa uchumi kutokana na umahiri wa usimamizi wa shughuli zake za kiuchumi ikilinganishwa na mataifa mengi ya kiafrika na ulimwengini kwa ujumla. 

Katika kikao chao, Dk. Nchemba na Dk. Nchemba walijadiliana kuhusu fedha hizo ambazo mkataba wake ulitiwa saini Juni 2, 2024 nchini Korea na kushuhudiwa na marais wa nchi hizo mbili. 

Pia walijadiliana kuondoa changamoto ya utozaji kodi mara mbili na ukwepaji kodi kwa kampuni zinazowekeza katika nchi hizo mbili pamoja na kuvutia uwekezaji.