CHADEMA Singida wamkana mwenyekiti wao

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 08:39 AM Jan 11 2025
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Singida Mjini, Swahibu Mohamed.
Picha:Mtandao
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Singida Mjini, Swahibu Mohamed.

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Singida Mjini, Swahibu Mohamed, amesema si kweli kwamba wajumbe wote 29 wa mkutano mkuu kutoka Mkoa wa Singida wanamuunga mkono mgombea uenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mohamed alisema kikao kilichoitishwa juzi Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Singida, Omari Toto, na kutoa tamko kwamba wajumbe wote 29 ambao ni wajumbe watakaopiga kura  katika mkutano mkuu utaofanyika Januari 21, wanamuunga mkono Lissu  si za kweli. 

Kauli hiyo ya Mohamed  imekuja siku moja tu baada ya Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa kutoa tamko kwamba mkoa unamuunga mkono Lissu. 

"Mkutano tulioitiwa na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa tuliambiwa ni wa mashauriano lakini kwa sababu akidi ya wajumbe haijatimia tumeshangaa mwenyekiti anaita waandishi wa habari na kutoa tamko kwamba CHADEMA Mkoa wa Singida wanamuunga mkono Lissu," alisema. 

Mohamed alisema kwa mujibu wa katiba ya chama, wajumbe watakaopiga kura katika mkutano mkuu wa uchaguzi ni mwenyekiti, katibu na mjumbe wa mkutano mkuu kutoka kila jimbo  ambao wanafanya jumla ya wajumbe 29 kutoka mkoa wa Singida. 

Alisema mkutano huo uliofanyika juzi Singida mjini, wenyeviti na makatibu wa majimbo yaliyoko mkoa wa Singida hawakuwapo, hivyo linapotolewa tamko kwamba wajumbe wote wa Singida wanamuunga mkono Lissu si kweli.

 Kwa mujibu wa Mohamed ambaye ni mlinzi wa Mbowe,  kati ya wajumbe 29 wanaotoka Mkoa wa Singida ana uhakika wajumbe 20 wanamuunga mkono Freeman Mbowe.

Juzi, Toto akitoa tamko, alisema sababu zinazowafanya wamuunge mkono Lissu ni kutokana na  suala la fedha za ruzuku zinazotolewa kwa chama. 

Toto alisema CHADEMA kila mwezi kimekuwa kikilipwa Sh. milioni 107 kama ruzuku ya chama lakini katika hali ya kushangaza fedha hizo zimekuwa zikiishia makao makuu bila kupelekwa mkoani kwa ajili ya maendeleo ya chama.

 "Fedha za ruzuku ambazo zinatolewa kwa ajili ya chama tunaimani Lissu akishakuwa Mwenyekiti  mgawanyo utakuwa unakuja hadi huku mikoani kwa ajili ya shughuli za chama tofauti na sasa ambapo zinaishia makao makuu tu," alisema.

 Alisema propaganga zinazoenezwa kwamba Lissu anaungwa mkono na wanachama ambao si wapigakura ni uongo na wanamdanganya Mbowe lakini kimsingi mfano katika mkoa wa Singida asilimia 75 Lissu anaungwa mkono.