KUMEKUWA na wimbi kubwa la wanamichezo duniani kuingia katika michezo ya kubashiri na katika hilo, Shirikisho la Mpira wa Miguu duniani (FIFA), limekiri kwa sasa hilo ni tatizo kubwa, kwani limekuwa likififisha burudani, hivyo linalifanyia kazi ili kudhibiti kundi hilo.
Hata hivyo, FIFA imekiri kuwa inapata wakati mgumu kwani wakati mwingine wanamichezo hao hawabashiri wao moja kwa moja, bali wanashirikiana na raia wa kawaida na hata makampuni kwa ajili ya kuangalia maslahi yao.
Kwa mujibu wa kanuni za FIFA wanamichezo, kama vile wachezaji, waamuzi, makamisaa, viongozi wa klabu, makocha na mashirikisho, hawaruhusiwi kujihusisha katika michezo ya kubashiri kwani wakifanya hivyo wanaweza kuathiri matokeo ya michezo yenyewe uwanjani.
Tunajua wenzetu Ulaya wameendelea, wana vyombo na teknolojia ya hali ya juu kubaini wanamichezo ambao wanajishughulisha na kubashiri na tumesikia mara kwa mara wakiwabaini wachezaji, waamuzi na viongozi kabla ya kuwapa adhabu.
Pamoja na hayo bado FIFA wanakiri hadharani hali ni ngumu, kwani baadhi yao hawajihusishi moja kwa moja, wanapitia kwenye migongo ya watu wengine, hivyo ni ngumu sana kupata ushahidi.
Hivi karibuni tumemsikia Ofisa Mtendaji wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Almasi Kasongo, akiulizwa maswali na baadhi ya waandishi wa habari kuhusu kuibuka kwa wanamichezo wa Tanzania nao kujihusisha na kubashiri.
Kasongo alisema wamesikia vitu kama hivyo, na akakiri kuwa jambo hilo linawasumbua hata huko Ulaya kwani halijawahi kuwa na ushahidi wa moja kwa moja, lakini tayari kuna kanuni ya kuwakataza wanamichezo kujihusisha na michezo hiyo ya kubashiri.
Alisema mpaka sasa hawajaliona, lakini kwa sababu wapo kwenye jamii, wanasikia vitu kama hivyo na kuahidi kulifuatilia kwa karibu.
Tunampongeza Kasongo kwa uthubutu wake, si wa kuonekana kupinga suala hilo, lakini pia kuahidi kuchukua hatua kama watapata ushahidi.
Hatupingi kwa TPLB na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), kuanza kudili na wanamichezo wanaobashiri, lakini tunaona kunatakiwa ushirikiano mkubwa kwa wapenzi wote wa soka.
Tunadhani levo yetu kwa sasa ni kudili na upangaji wa matokeo kwanza ambao ndio unasikika na unaweza kupatikana ushahidi kama vyombo vyetu vitakuwa na dhamira ya dhati kwa hilo.
Kuwapo kwa kampuni moja inayodhamini klabu zipatazo sita kwenye Ligi Kuu huku moja kati ya hizo ikiweka mkono mkubwa zaidi, ni dalili mojawapo kuwa hatuko salama sana kwenye upangaji wa matokeo.
Bado kuna timu zinaahidiwa kiasi cha pesa zinapocheza na baadhi ya timu tu, huku zikicheza na zingine huwezi kusikia hilo, hizi zote si dalili njema kwenye mpira wetu.
Na kwa bahati nzuri haya yote hayahitaji teknolojia ya hali ya juu kudhibiti, badala yake ni kusimamia misingi wa 'fair play' kuwa kampuni ambayo ina maslahi na timu moja isiruhusiwe kuzidhamini zingine, kuondoka ahadi za ujanjaujanja za pesa timu zikicheza na timu fulani, badala yake kama zinataka ziwekwe zinapocheza na timu zote kubwa, pamoja na kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa ajili ya kubaini waamuzi wanaopokea rushwa, wachezaji na hata viongozi wanaotoa kwa timu zingine.
Tunaamini hili linawezekana kama tukiwa na nia ya dhati kuliko la kubashiri. Bado kuna matatizo ya msingi sana kwenye soka letu ambayo hajapatia ufumbuzi kama haya. Tukiondoka huku tunadhani ndiyo twende kwa wanaobashiri. Wenzetu wameshaondokana na mambo ya kuuza au kununua mechi, ndiyo maana wameelekeza nguvu zao sasa huko.
Tuanze kwanza na tuhuma za kuuza na kununua mechi, pamoja na rushwa kwa waamuzi, haya ndiyo matatizo yetu ya msingi, mambo ya wanaobeti sawa yapigwe vita, TPLB ikiweka mkazo kwanza kwenye kilio cha udhamini huu ambao umekuwa ukipigiwa kelele kuwa na viashiria vya upangaji matokeo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED