Shule yaweka wanafunzi njiapanda

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:52 AM Jan 07 2025
Shule yaweka wanafunzi njiapanda.
Picha:Maktaba
Shule yaweka wanafunzi njiapanda.

ZIKIWA zimesalia siku tano pekee shule kufunguliwa kwa muhula wa kwanza wa mwaka 2025, wazazi na wanafunzi zaidi ya 600 wako njiapanda, baada ya moja ya shule kudaiwa kuwafukuza na kuwataka wahamishe wanafunzi.

Taharuki imeongezeka zaidi kutokana na uongozi wa shule kutoitisha kikao cha wazazi, badala yake mawasiliano yote yanafanyika kwa ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu za kiganjani (SMS), kutoka shuleni kwenda kwa wazazi.

Baadhi ya wazazi waliozungumza na Nipashe jana, walisema badala ya shule kuitisha kikao, Ijumaa iliyopita Januari 3, 2025, Kaimu Mkuu wa Shule ya Rainbow, Denis Mbiro, alituma ujumbe kwa wazazi ukisisitiza wahamishie wanafunzi shule jirani.

UJUMBE 

Ujumbe huo wa maneno 157, ambao mwandishi wa habari hii amefanikiwa kuuona na kuthibitishwa na Kaimu Mkuu wa Shule ya Rainbow unasomeka kwamba: “Ujumbe muhimu. Heri ya Mwaka Mpya.” 

“Uongozi wa Kanisa la Tanzania Presbyterian Church (TPC), unapenda kuwajulisha wazazi wa wanafunzi wa shule ya Hephzibah- upande wa shule ya msingi kuwa, tayari umeshafikia makubaliano na shule mbili, ambazo ni Joyland International School inayopatikana upande wa pili wa Fun City na Taneem Schools inayopatikana Toangoma kuwapokea wanafunzi wetu na kuendelea kupata huduma ya elimu mpaka ukarabati na ujenzi utakapokamilika.

Tunatambua wapo wazazi ambao walishapata shule za watoto wao kuendelea na masomo. Hivyo tunawaruhusu kuendelea pasipo kuleta mkanganyiko. Kwa wale ambao wamepata changamoto, wanaweza kuchagua moja kati ya hizi na mtoto atapokewa bila shida yoyote.

Shule zote mbili zitafunguliwa Jumatatu tarehe 13/1/2025. Tunaomba wazazi mfike kwa ajili ya taratibu za watoto kujiunga na shule.

Pia tumewasilisha majina ya wanafunzi wote katika shule zote mbili, mzazi unaweza kuchagua yeyote kati ya hizo. Mungu awabariki sana.”

Awali, uongozi wa shule hiyo ya Awali na Msingi, Rainbow inayomilikiwa na Kanisa la Tanzania Presbyterian Church (TPC), ambayo ipo Kata ya Toangoma, wilayani Temeke, ilitangaza kufunga kwa mwaka mmoja na nusu kuanzia Januari mwaka huu, kwa kutuma SMS kwa wazazi na walezi wa wanafunzi.

Wakizungumza na gazeti hili jana, baadhi ya wazazi na walezi walisema baada ya kupokea ujumbe huo, waliomba uongozi uitishe kikao kutafuta njia ya kuwasaidia wanafunzi ili wasiathirike kimasomo, lakini uongozi umekataa kufanya hivyo.

Mzazi mwenye watoto wawili shuleni hapo, Magreth Laurent, alisema Desemba 6, mwaka jana, Meneja wa Shule za TPC, Mchungaji Hallington Kamanga, aliwatumia ujumbe mfupi akieleza sababu za kufunga shule kuwa ni ukarabati wa majengo.

Hata hivyo, alisema wazazi waliomba uongozi uitishe kikao cha pamoja na uongozi uliahidi kuitisha, bila kutekeleza.

“Hata tukiwapigia hawapokei na tulivyoenda kuomba kikao cha wazazi walisema watatupigia na badala yake wanatutumia meseji. Tunajiuliza serikali yetu inawaangalia watoto wa Tanzania wakinyanyaswa kiasi hiki kweli?” Alihoji.

Kwa mujibu wa wazazi hao, uongozi wa kanisa na wa shule hiyo, umekuwa na utaratibu wa kutuma ujumbe mfupi kwa wazazi na walezi kwa taarifa zinazohitaji mwafaka wa pamoja.

Ujumbe wa awali kutoka kwa Meneja wa Shule za TPC, Mchungaji Kamanga, ulisema shule ya Rainbow inafungwa kupisha ujenzi na maboresho ya majengo.

Mzazi mwingine, Dk. Lilian Isack, alisema wazazi waliomba wanafunzi hao wahamishiwe kwenye shule nyingine za TPC, pendekezo ambalo limepingwa na kanisa hilo.

“Ni kitu cha ajabu sana kwa kweli, tunajiuliza kwa nini wanawafukuza watoto kabisa? Wana shule nyingine, lakini hawawataki kabisa hawa watoto, tunajiuliza hawa ni wamishionari gani?”

Akizungumza na Nipashe jana, Mwalimu Mbiro alisema wamelazimika kuifunga shule hiyo ili kuboresha majengo na kuanza upya, kutokana na kupungukiwa na wanafunzi.

“Kanisa liliipokea shule mwaka jana ikiwa na idadi ndogo ya wanafunzi kiasi kwamba hatuwezi kuendelea kuiendesha na ndio maana tunaifunga kwa muda,” alisema.

Alipoulizwa sababu za kutoitisha kikao cha wazazi badala ya kutuma ujumbe huo, Mbiro alijibu kwa kifupi kwamba hayo ni mawasiliano rasmi kutoka shuleni.

“Tuliwapa wazazi nafasi ya kuomba kujiunga na shule yetu nyingine kwa utaratibu wa wanafunzi kufanyiwa usaili ili watoto wanaofaulu wahamie kwetu, wapo waliofanikiwa. Kwa sasa tumefunga usaili na tumeingia makubaliano ya shule nyingine ambazo watoto wanaweza kuhamia hata bila usaili,” alifafanua.

Alisema shule hiyo inafungwa baada ya kanisa kushinda kesi ya madai namba 28/2022, iliyofunguliwa na wachungaji Jung Hwan Kim na Sang Ok Nam, waliokuwa walalamikaji dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya TPC, waliokuwa washtakiwa.

Baadhi ya wazazi waliiambia Nipashe kwamba uamuzi huo umekuja ghafla kwa kuwa Septemba, mwaka jana walisikia tetesi za shule hiyo kufungwa, lakini walipofuatilia kwa nyakati tofauti, uongozi wa shule na wa kanisa ulikanusha na kudai ni uzushi, huku wakiwataka waupuuze.

“Kufukuza mtoto wa darasa la kwanza bila huruma ni kutojali taifa la kesho. Tunaiomba serikali iwasaidie watoto hawa wasio na hatia, wapate haki yao ya elimu,” alisema Dk. Lilian.

KESI 

Nakala ya hukumu ya kesi hiyo, ambayo Nipashe imeiona, ilitolewa Februari 5, mwaka huu na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, John Nkwabi, aliyeirejesha shule mikononi mwa kanisa. Katika kesi hiyo, upande wa walalamikaji uliwakilishwa na Wakili Hamis Mbangwa na walalamikiwa uliwakilishwa na Wakili Paschal Kamala.

Hata hivyo, licha ya Kanisa kurejeshewa shule tangu Februari, uongozi wa kanisa haukuichukua shule hadi Septemba, mwaka jana.

Baadhi ya wazazi wamedai kuwa miezi minane ya TPC kutoingiza menejimenti mpya shuleni Rainbow sasa Hephzibah, ulilenga kuwawezesha walalamikaji, Jung Hwan Kim na Sang Ok Nam, kujenga shule mpya.

Mmoja wa wazazi mwenye wanafunzi shuleni hapo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alidai kuwa kilichotokea ni hujuma dhidi ya kizazi cha Tanzania kwa kuwa TPC ilishirikiana na menejimenti ya zamani kuwezesha ujenzi wa shule mpya katika eneo la Kisarawe II, lililoko Kata ya Kisarawe, Kigamboni mkoani Dar es Salaam, ambayo imesajiliwa kwa jina la Rainbow Junior Christian.

Anasema kutokana na jina la Rainbow kuhamia Kisarawe II, TPC imelazimika kuibadilisha shule ya Toangoma jina na kuiita Hephzibah.

Wiki iliyopita, Kamishna wa Elimu Tanzania, Dk. Lyabwene Mtahabwa, alisema kilichofanyika shuleni hapo ni kinyume cha utaratibu, kanuni na mwongozo wa shule, unaotaka haki ya mtoto ilindwe katika mazingira yoyote.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Mtahabwa amewaelekeza wadhibiti ubora kwenda kukagua shule hiyo ili kubaini chanzo cha kufungwa kwake. Hata hivyo, jana mwandishi wa habari hii alimtafuta Kamishna bila mafanikio baada ya simu yake kuita bila kupokewa.