UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya mauaji inayowakabili watuhumiwa watano, umewasomea upya shtaka hilo kwa kuwaunganisha watuhumiwa wote watano.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Diwani wa Nyanzwa, Boniphace Katili, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM ) Wilaya ya Kilolo, Hedikosi Kimwaga na wenzao watatu.
Wote kwa pamoja walifikishwa tena mahakamani jana saa 3:47 asubuhi kwa magari mawili; aina ya Landa Cruiser yenye namba za usajili PT 1909 na KM 91 MS -GP yaliyosindikizwa na askari waliobeba silaha mbalimbali na mabomu ya machozi.
Kwa muda wote kabla ya watuhumiwa hao kufikishwa mahakamani, wananchi wakiwamo ndugu wa marehemu, viongozi wa jumuiya za CCM na makada wa vyama mbalimbali na wasio na vyama, walijitokeza kufuatilia kesi hiyo tofauti na siku ya kwanza ambayo walikuwapo ndugu wa watuhumiwa pekee ambao hawakuzidi 10.
Washtakiwa walifikishwa mahakamani huko jana mbele Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, Rehema Mayagilo kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo, Christina Kibiki.
Washtakiwa wote ni Kefa Wales, Silla Kimwaga, Boniphace Katili, Willy Chikweo na Hedikosi Kimwaga.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Sauli Makori alidai mahakamani huko kuwa mshtakiwa namba moja katika kesi hiyo, Wales, alifikishwa mahakamani na kusomewa shtaka hilo pekee yake kabla ya watuhumiwa wengine wanne kusomewa shtaka hilo, hivyo akaomba kusoma upya maelezo ya shtaka kwa watuhumiwa wote watano.
Akisoma upya maelezo ya kesi hiyo ya jinai namba 34404 ya mwaka 2024 ya mauaji, alidai kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Novemba 12, 2024 katika kijiji cha Ugwachanya, wilayani Iringa. Hata hivyo alisema upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Hakimu Rehema alisema watuhumiwa hawapaswi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo kisha akaiahirisha hadi Januari 21 mwaka huu saa tatu asubuhi itakapotajwa tena.
Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, wakati watuhumiwa hao na wengine wakipandishwa kwenye gari kuelekea mahabusu gerezanim, baadhi ya washtakiwa wa kesi zingine walisikika wakipaza sauti kuwapongeza waandishi wa habari kwa kutimiza wajibu wao.
"Kazi nzuri... kazi nzuri waandishi... pigeni kazi..." walisikika baadhi ya washtakiwa hao wakati wakiingizwa katika moja ya magari yaliyotumika jana kuwafikisha mahakamani washtakiwa wa kesi hiyo ya mauaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED