JESHI la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia John Isaya (21), dereva bajaji na mkazi wa Mtaa wa Bukala, wilayani Sengerema kwa tuhuma za kutengeneza na kusambaza picha mjongeo katika mtandao wa kijamii wa Tik Tok, akitangaza kuwa anauza mtoto wake aliyekuwa amembeba kwa mbeleko kwa Sh. million 1.6.
Taarifa ya kukamatwa kwa Isaya ilitolewa juzi na Kamanda wa Polisi mkoani hapa, DCP Wilbrod Mutafungwa wakati anazungumza na vyombo vya habari na kutaja kitendo hicho kuwa ni kinyume cha sheria na ni ukatili kwa mtoto huyo.
Kamanda Mutafugwa alisema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kumetokana na taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi hilo Makao Makuu Dodoma, DCP David Misime.
Alisema kuwa taarifa ya DCP Misime ilielekeza mtu huyo atafutwe na akamatwe ili awajibike kisheria kwa kitendo alichokifanya Januari 4, 2025 kilichotweza utu na kukiuka haki ya mtoto huyo.
DCP Mutafungwa alisema kufuatia mahojiano yaliyofanyika dhidi ya mtuhumiwa huyo, chanzo cha tukio hilo ni kutafuta umaarufu kupitia mitandao ya kijamii.
"Tunawakumbusha wananchi kuendelea kufichua vitendo vya kihalifu na waendelee kuvilaani na kuvikemea vitendo vya ukatili wa aina zote kwani vinaweza kusababisha madhara kwa watoto na vinadhalilisha na kushushia thamani utu wao," alisema Kamanda Mutafungwa.
Akikemea tukio la maudhui ya kuuza mtoto juzi, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Dorothy Gwajima, aliwataka waandaaji maudhui mtandaoni kuzingatia weledi ili kuepuka uvunjifu wa maadili ya kijamii.
"Jamii ya watanzania inastahili kujipambanua kwa heshima na kuheshimu makundi ya rika zote yanayofanya shughuli mbalimbali za haki mitandaoni, yanastahili heshima na staha," alisema Dk. Gwajima.
Katika hatua nyingine, Kamanda Mutafungwa alisema jeshi hilo linamshikilia Doto Sita (32), fundi ujenzi na mkazi wa Kishiri, jijini Mwanza kwa tuhuma za kumnajisi na kumlawiti mtoto wake wa kambo mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu hadi kumsababishia umauti.
Kamanda Mutafungwa alisema mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda ukatili dhidi ya mtoto huyo mara kwa mara huku mama mzazi wa mtoto huyo, akiwa anajua kilichokuwa kinaendelea lakini hakutoa taarifa mpaka wasamalia wema walipotoa taarifa hiyo kwa polisi.
"Raia wema walitoa taarifa hiyo polisi kupitia dawati la jinsia na watoto ambao walifika haraka eneo la tukio na kumkuta mtuhumiwa akishirikiana na mke wake Aneth Mhano (23) kufanya jitihada za kumpeleka hospitalini mtoto huyo ili apatiwe tiba ambako hata hivyo alifariki dunia wakati akiendelea na matibabu," alisema Kamanda Mutafungwa.
Alisema kuwa walifika Kituo cha Afya Usumau ambako walielekezwa kumpeleka mtoto huyo katika zahanati ya serikali Igoma, wakiwa katika harakati za matibabu katika zahanati ya Igoma, mtoto huyo alifariki dunia.
Alisema kuwa mbali na kumkamata mtuhumiwa huyo, pia wanamshikilia na kuendelea kumhoji mama mzazi wa mtoto huyo kwa kutotoa taarifa kwa Jeshi la Polisi au kwa jirani zake juu ya ukatili aliokuwa anafanyiwa mtoto ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Alisema tayari mwili wa mtoto umefanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kisha kukabidhiwa kwa baba yake mzazi, Emmanuel Daudi (28) na ndugu wengine kwa ajili ya mazishi na kuwa uchuguzi wa tukio hilo unaendelea na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kuhusika katika kutekeleza ukatili huo ambao umesababisha kifo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED