MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche amekoleza moto katika mnyukano unaoendelea wa wanachama na wafuasi wa chama hicho.
Hii ni baada ya kuchukua na kurejesha fomu ya kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Taifa huku akiweka wazi kuwa anamuunga mkono Tundu Lissu katika mbio za kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa.
Vilevile, Heche aliyewahi kuwa Mbunge wa Tarime kwa tiketi ya CHADEMA, pia amewataka wajumbe wa Kamati Kuu kusikiliza alichokiita "sauti za wanachama".
Heche alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, wanachama na waandishi wa habari kuhusu nia yake ya kuwania nafasi hiyo.
Aliwataka wajumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA kuhakikisha wanasikiliza sauti ya wanachama na kufanya uamuzi sahihi bila kufuata mahitaji yao binafsi wakati wa uchaguzi wa viongozi wakuu wa chama hicho mwezi huu.
"Mkienda na matamanio yenu na kusikiliza vichwa vyenu na matumbo yenu, wanachama hawatowaelewa miaka yote," Heche aliwaonya.
Alisema kuwa katika kuwania uongozi ndani ya chama hicho, yeye anamuunga mkono Lissu, mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti Taifa kutokana na mrengo wake wa kutaka haki, ukweli na uwazi ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Heche alisema 'Kambi ya Lissu' wana uhakika wa kuchukua kiti na kuongoza chama hicho na kuwa hawako tayari kuona kinaongozwa na malengo ya watu binafsi kinyume cha madhumuni ya kuanzishwa kwake.
"Chama hiki kimeanzishwa kwa madhumuni maalumu ikiwa ni pamoja na kushinda dola na kuiondoa CCM (Chama Cha Mapinduzi), kulinda na kutumia rasilimali za nchi kwa manufaa ya watanzania, kuwapatia huduma bora watanzania ikiwa ni pamoja na matibabu, elimu na umiliki wa rasilimali binafsi," Heche alisema.
Alisema kuwa watu wengi wamefariki dunia kwa namna tofauti katika kuhakikisha wanapigania maslahi ya chama hicho, hivyo hawako tayari kuona kinaongozwa kwa malengo binafsi.
UCHAGUZI MKUU
Kuhusu chama hicho kushiriki Uchaguzi Mkuu mwaka huu, Heche alisema wakipata nafasi hiyo hawatakubali kushiriki bila kuwa na mabadiliko ya Tume ya Uchaguzi.
"Tutapeleka nguvu ya umma na tuna imani watasimama na sisi kama walivyosimama nasi katika mabadiliko mbalimbali kuhakikisha tunashinikiza serikali kufanya mabadiliko ya Tume ya Uchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu na tutasimama katika msimamo wetu kuwa 'no reform no election' (hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi," alisema Heche.
KUKICHAFUA CHAMA
Kuhusu madai kwamba Lissu anachafua chama, Heche alisema anaunga mkono kampeni za Lissu kuwasema na kuibua kashfa za baadhi ya watu wanaodaiwa kupokea rushwa ndani ya chama hicho.
"Kuna watu wanachafua viongozi wengine, wanamwita Lissu muongo, si kweli! Lissu ni mkweli na mtu safi. Yeye anachokifanya ni kuwavua nguo wanaovua nguo chama na wala si chama chenyewe.
"Wananchi wakikwambia wanataka mchicha ukawaletea vitu vingine kwa madai zote ni mboga za majani, hawatokuelewa," alisema Heche.
Heche pia alisema anamheshimu Mwenyekiti wa sasa, Freeman Mbowe kama baba yake na mlezi wa kisiasa na kuwa haitotokea kumkosea heshima. Anao mchango mkubwa katika demokrasia ya taifa na chama chao.
Baadhi ya wananchi mkoani Mwanza, akiwamo Anthelius Audax walisema kuwa kwa sasa chama hicho kimekua, hivyo viongozi wake wanahitaji kuwa makini ili kuhakikisha wanamaliza uchaguzi wao wa ndani bila kuwa na mvurugano ambao utasababisha mpasuko.
Wakati dirisha la kuchukua fomu ya kuwania uongozi ndani ya chama hicho kitaifa likifungwa jana, John Heche anakuwa mshindani wa pili katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti, akitanguliwa na Ezekia Wenje aliyechukua na kurejesha fomu Januari 3 mwaka huu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED