RAS atoa agizo kali Soko Tandale

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 06:34 PM Jan 07 2025
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Toba Nguvila.
Picha:Mpigapicha Wetu
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Toba Nguvila.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Toba Nguvila, ametoa siku 14 kwa watendaji husika kuhakikisha changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa Soko la Tandale zinamalizika na kuweza kuanzishwa huduma ya biashara kwa saa 24.

 Agizo hilo amelitoa alipokutana na viongozi wa soko hilo na kuwataka kukamilisha hatua zote muhimu kwa kufikia malengo hayo.

Dk. Nguvila amesisitiza kuwa changamoto zinazohitaji kutatuliwa kabla ya Januari 20, 2025, ni pamoja na kuboresha mfumo wa taa za sokoni, ambazo wafanyabiashara wamekuwa wakilalamikia kuwa hazina mwanga wa kutosha. Ameelekeza kuwa taa kubwa zaidi zikanunuliwe ili kuboresha mazingira ya kazi, na pia kuwawezesha wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa usalama hata usiku.

Aidha, ametaja haja ya kununua jenereta kubwa litakalohudumia soko hilo kwa saa 24, ili kuhakikisha huduma za umeme zinaendelea hata wakati wa umeme kukatika. Dk. Nguvila pia amesisitiza ununuzi wa pampu za kuvutia maji ili kutatua changamoto ya uhaba wa maji, na kero ya mafuriko yanayoathiri baadhi ya vizimba wakati mvua zinaponyesha.

Mbali na hayo, Katibu Tawala ameagiza Katibu Tawala wa Manispaa ya Kinondoni na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, wakutane na LATRA ili kupanga ruti za mabasi zitakazoweza kufika kwenye soko hilo na hivyo kufikisha huduma kwa urahisi zaidi kwa wananchi na wafanyabiashara. Ametoa hadi Januari 10, 2025, kwa kujua lini ruti hizi zitaanza.

Katika hatua nyingine, Mweka Hazina wa Manispaa ya Kinondoni, Onesmo Mwonga, amesema kuwa mara baada ya changamoto hizo kutatuliwa, soko hilo litakuwa na uwezo wa kuzalisha mapato ya Shilingi Milioni mbili na laki tano kwa siku, na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye maendeleo ya kiuchumi ya eneo hilo.

Wafanyabiashara wa soko hilo wamesikitishwa na hali ya mwanga hafifu, ukosefu wa barabara za kuingilia kwa magari, na changamoto ya mafuriko yanayotokea wakati wa mvua. Wameelezea pia wasiwasi wao kuhusu ukosefu wa vyoo katika ghorofa ya chini, jambo ambalo linazidi kuzidisha kero kwa jengo hilo jipya.

Katika ziara hiyo, Dk. Nguvila pia alikagua Kituo cha Afya Kinondoni, ambacho kimekamilika na kuanza kutoa huduma za afya kwa mama na mtoto, maabara, na huduma za wagonjwa wa nje. Kituo hicho kina watumishi 32, na kuna mapungufu ya watumishi 20, ambapo kibali cha ajira kimeshatolewa.

Pia amekagua mradi wa jengo jipya la Manispaa ya Kinondoni, ambalo limekamilika kwa asilimia 98. Ameagiza Mkurugenzi na Meya wahamie katika jengo hilo haraka, huku akitolea wito idara nyingine zilizobaki kuhamia pia ili kuimarisha utendaji kazi wa ofisi na kuongeza mapato kupitia matumizi bora ya jengo la zamani.

3