Walemavu, wazee, yatima, wajane wasikumbukwe kwa sikukuu pekee

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:00 PM Jan 03 2025
Walemavu, wazee, yatima, wajane wasikumbukwe kwa sikukuu pekee.
Picha: Mtandao
Walemavu, wazee, yatima, wajane wasikumbukwe kwa sikukuu pekee.

KUMEKUWA na utaratibu mzuri tu nchini kwetu wa watu binafsi, taasisi mbalimbali na hata wanasiasa kuwakumbuka watu wenye uhitaji wakati wa sikukuu.

Tumekuwa tukiona sikukuu nyingi kama vile Krisimasi, Mwaka mpya, Pasaka, Idd El Fitri, Idd El Hajji, taasisi na watu wengine wakimiminika kutoa misaada mbalimbali ya chakula, nguo, vinywaji, mbuzi, ng'ombe, kuku na vingine vinavyofanana na hivyo.

 Watu wenye mahitaji ambao ninawazungumzia hapa ni watoto yatima, wajane, wazee, na hata watu wenye ulemavu ambao kipindi hicho wamekuwa wakipata faraja ya msaada na kutembelewa pia.

 Hiki ni kitu kizuri sana kwa sababu kinawafanya wahitaji hao ambao wakati mwingine wanaona kama wametengwa na jamii kujiona kuwa ni sehemu yao.

 Mara nyingi yeyote anayeona ametengwa na jamii hukosa kujiamini na wakati mwingine hasa watoto baadaye anaondokea kuwa katili na kufanya mambo yasiyofaa kutokana na kile ambacho anaona kama ni kulipiza kisasi kwani kwenye makuzi yake aliona kama jamii ilikuwa imemtenga.

 Watu wanaokwenda kutoa misaada kitu ambacho wanatengeneza kwa wahitaji hao ni kuwapa faraja, kuwafanya kuondokana na mawazo potofu ya kutengwa au kujitenga wenyewe, wakati mwingine kuwafanya waanze kujiamini kwani anaanza kujiona ni watu kama wengine tu.

 Kwa siku za karibuni tumeona hata klabu za mpira kama vile Simba, Yanga, Azam, na zingine za ligi kuu zimeanzisha utaratibu huu.

 Zikitaka kuanza kucheza Ligi Kuu, yaani kabla ya msimu mfano Simba Day, au Siku ya Mwananchi, hufanya shughuli za kijamii ikiwamo kutembelea wahitaji, wagonjwa mahospitalini na hata kutoa damu.

 Hili ni jambo zuri na linapaswa lipongezwe na liendelee kwa watu wote kwani lina faida nyingi ambazo nimezieleza. 

 Hata hivyo ushauri wangu ni kwamba tusiwaache peke yao mpaka siku za sikukuu tu ndiyo taasisi na watu waanze kufuatana kwenda kutoa misaada na kuwaangalia.

 Nadhani sasa Watanzania tuanze kuwa na utamaduni wa kwenda kuwaangalia mara kwa mara, kutoa misaada kula nao chakula na kuwafariji.

 Tunaambiwa kwenye dini zote kuwa unapotoa kwa watu wenye uhitaji kama hao kwa asilimia 100, basi unapata thawabu kubwa, hivyo uwepo utamaduni wa mtu mmoja mmoja, familia, au vikundi kuchangishana pesa na kwenda kuwatembelea kuwapa msaada na kuwafariji.

 Wahitaji hao wasizoee kuona mpaka ikifika sikukuu ndiyo waanze kuona wageni wakimiminika.

 Waanze kuzoea kupokea wageni mara kwa mara hata kama siyo siku za sikukuu, na ikifika wakati huo ndiyo waongezeke zaidi.

 Kuna vitu vingi vya kujifunza iwapo yeyote atakwenda kuwatembelea wazee, yatima, wajane, wafungwa, hata walemavu, kama ambavyo baadhi wanavyojifunza wakienda kutembelea wagonjwa hospitalini.

 Ifanywe kama sehemu ya mtoko, kama vile wanaokwenda baa, klabu, ufukweni au 'pikniki'.

 Siku hizi kuna vikundi vingi, vikiwemo vya kusaidiana, kutenga wikiendi moja kwenda kutoa msaada, kushinda na kula na watu wenye mahitaji ni jambo litawafanya kuwa na amani ya moyo.

 Niwapongeze Watanzania wote ambao wamekuwa na utamaduni wa kuwasaidia na kuwatembelea nyakati za sikukuu. Ushauri wangu sasa waanze kutembelewa sasa hata siku za kawaida ili wakati mwingine kujua shida zao za kila siku zinazowakabili.