Matukio kuhusu ukatili yamalizwe kwa vitendo

Nipashe
Published at 01:18 PM Dec 27 2024
Matukio kuhusu ukatili yamalizwe kwa vitendo
Picha:AI
Matukio kuhusu ukatili yamalizwe kwa vitendo

VITENDO vya ukatili vimekuwa vikishamiri siku hadi siku katika jamii huku jitihada za kutokomeza zikiwa zinaendelea. Vitendo hivyo, kila uchao vimekuwa vikisikika na kuripotiwa kwenye vyombo vya habari nchini.

Miongoni mwa vitendo hivyo, ni mauaji baina ya wanandoa yanayosababishwa na wivu wa kimapenzi, msongo wa mawazo na mmomonyoko wa maadili huku kwa sehemu kubwa, wanaume wakionekana ndio wahusika wakubwa kwa kuwaua wake zao na watoto pia. Wako wengine ambao wameripotiwa kuwanyonga, kuwachinja wenza wao kisha kuwafukia.

Yako pia baadhi ya matendo yaliyoripotiwa kwa baadhi ya kinababa kudaiwa kuwaua wake na watoto wao kwa madai vipimo vya vinasaba kuonesha kuwa si watoto wao. Iko pia taarifa iliyoripotiwa kuwa mume alimuua mke wake baada ya kukuta amepikiwa nyama wakati aliacha fedha kwa ajili ya maharage na mboga ya majani? Kwa kukuta chakula hicho, mawazo yalimfikirisha kwamba amepewa na mwanamume wake wa pembeni!    

Kwa ujumla, matukio hayo yanazidi kuwa tishio katika jamii licha ya wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa serikali, wa dini, wanaharakati na vyombo vya habari kukemea siku kwa siku. Machi, mwaka huu, kwa mfano, katika kikao cha kujadili vitendo vya ukatili wa kijinsia, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, alisema matukio ya ukatili mkoani humo yamefikia 8,360 hadi Desemba, 2023. 

Takwimu hizo zinaonesha kwamba matukio hayo yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku jambo ambalo linaonensha kwamba watu sasa hawana hofu ya Mungu. Wanadiriki kuwafanyia unyama binadamu wenzao bila huruma na hata kuwasababishia vifo na ulemavu wa kudumu.

Hali hiyo pia imewafanya binadamu kuwa zaidi ya hayawani na kuondoa uhalisia kwamba waliumbwa kwa mfano wa Mungu, hivyo wanapaswa kutenda mambo mengi yakiwamo matendo ya huruma. 

Moja ya matukio yaliyoripotiwa katika gazeti hili ni mwanamke mmoja, aliyejulikana kwa jina la Maria Maladukwa (42) mkazi wa kijiji cha Ghidika mkoani Manyara, kutoroka nyumbani kwake na kukimbilia mkoani Singida kwa madai ya kufanyiwa ukatili wa kijinsia na mume wake. 

Kwa mujibu wa habari hiyo, inadaiwa kuwa mume wake huyo alimfunga seng'enge na nondo ndogo katika miguu yake kama mtumwa kwa miezi miwili, hivyo kumsababishia maumivu na kudhoofika mwili kutokana na mateso aliyodai kupewa na mwenza wake huyo.  Kutokana na mateso hayo, mwanamke huyo alifika katika Kijiji cha  Matumbo, wilaya ya Singida huku akiwa na seng'enge katika mguu wa kushoto baada ya kutembea kwa saa 13 kutoka mkoani Manyara.

Kwa mujibu wa uongozi wa Kijiji hicho uliompokea mwanamke huyo, alidai kuwa  alifanikiwa kutoroka nyumbani kwake baada ya kukata  seng'enge alizokuwa amefungwa katika mguu wa kulia na kubakia na za mguu wa kushoto na alikimbia kwa nia ya kuwatafuta wazazi wake na kuomba hifadhi.  

Kwa jumla, matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto yamekuwa sawa na wimbo usio na mwisho katika masikio ya wanadamu kutokana na ukweli kwamba kila siku yamekuwa yakisikika. 

 Kutokana na ukweli huo, ni vyema sasa kila mwanajamii akasimama kwa nafasi yake kukemea vitendo hivyo ambavyo vinaiweka jamii ya Kitanzania katika taswira hasi na kuonekana kama ni mambo ya kawaida. Ni dhahiri kwamba kama vitendo hivyo vitaachiwa na kuendelea kushamiri, kuna athari kubwa za kijamii na kiuchumi ndani ya nchi. 

Kama ule msemo wa mapambano dhidi ya Ukimwi unavyosema ‘It Begins  With You’ kwa maana kwamba mapambano yanaanza na wewe, ni vyema sasa kila Mtanzania akafahamu kwamba mapambano dhidi ya ukatili yanaanzia kwake. Tanzania bila ukatili inawezekana.