Malasusa ahimiza malezi bora kwa watoto

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 10:21 AM Dec 27 2024
Malasusa ahimiza malezi bora kwa watoto
Picha:Mtandao
Malasusa ahimiza malezi bora kwa watoto

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa, amewahimiza wazazi na walezi kuwalea watoto wao katika misingi ya dini ili wakue na kuimarika kiimani baada ya kupata sakramenti ya Kipaimara.

Askofu Dk. Malasusa alisema hayo jana kwenye ibada ya kuwakumbuka wafia dini iliyofanyika KKKT Usharika wa Mbezi Beach, Dar es Salaam ambayo iliambatana na sakramenti ya kipaimara na ubatizo.

Aliagiza viongozi wa kanisa kuendelea kutoa elimu ya misingi ya kiimani kwa vijana hao ili wasiache njia ya imani yao.

“Mnaposali hakikisheni wanafunzi hawa waliopata mafundisho ya kipaimara mnaendelea kuwapatia elimu ya misingi ya kiimani ili  wasiache njia ya imani yao.

“Tunataka wanafunzi hawa waendelee kumtumikia Mungu na kuishi maisha ya imani waliyojifunza,” alisema.

Juzi akihubiri katika ibada ya Krismasi, katika Kanisa Kuu la Azania Front, Askofu Malasusa alionesha kusikitishwa na vijana kuwa nyuma katika suala la imani tofauti na ilivyo katika makundi mengine.

Alisema vijana wengi wakipata sakramenti muhimu wamekuwa hawana mwendelezo mzuri wa imani yao.

“Kwenye sakramenti kama hizi za kipaimara, huwa tunakuwa na vijana wengi, lakini baada ya hapo wengi huwa hawaonekani kanisani, ni vema kuendelea kuwafundisha vijana wetu kumpenda Mungu na kuwa watu wa imani,” alisema.

Akihuburi katika ibada hiyo, Askofu wa Kanisa la Morovian Jimbo la Mashariki,  Lawi Mwankuga, aliwataka Wakristo kuwa waamini katika kila jambo hasa katika mazingira ambayo wengine wanaweza kushindwa kuwa waaminifu.

“Mwenyezi Mungu atupe neema hata pale ambapo wengine wanaweza wakashindwa kuwa waaminifu, atujalie tuwe waaminifu, asubuhi, mchana na jioni, wewe wajibika kwa ajili ya taifa zima la Tanzania,”alisema Askofu Mwankuga.

Katika ibada hiyo,wanafunzi 30 wa usharika huo wa KKKT Mbezi Beach,walipatiwa sakramenti ya kipaimara.