MAKAMU Mwenyekiti wa Makanisa ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Mkoa wa Iringa, Askofu Dk. Blasston Gaville, ameipongeza serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ya kimkakati.
Dk. Gaville ambaye ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, alisema hayo juzi wakati akitoa salamu za Krismasi baada ya ibada ya kitaifa ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa Kuu la KKKT Dayosisi ya Iringa, mjini hapa.
Alisema CCT na waumini kwa ujumla wanaipongeza serikali kwa kazi kubwa zinazofanyika, zinazoonekana na hata zile zisizoonekana kwa macho ya kawaida.
Askofu Dk. Gaville alisema miradi mikubwa ya kimkakati kama ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na uendelezaji wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere ni mfano mzuri wa juhudi hizo.
Pia, aliipongeza Serikali kwa kuzindua vifurushi vipya vya bima ya afya kwa makundi mbalimbali, hatua inayolenga kuboresha afya za Watanzania wengi.
“Watanzania wenzangu, huu ni wakati wa kumwombea Rais wetu na serikali yake kwa ujumla. Utekelezaji huu wa miradi tunaouona haujafanyika kwa muda mrefu nchini. Hii ni fursa ya kuimarisha maendeleo na afya ya wananchi wetu,” alisema.
Askofu Dk. Gaville pia alisisitiza umuhimu wa kulinda na kutunza miradi hiyo, huku akiwataka Wakristo na Watanzania kwa ujumla kutambua mchango wa serikali katika kukuza sekta za elimu, afya, na uwekezaji wa kimkakati.
Pia aliwapongeza Watanzania wote walioshiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa amani, akiwahimiza wale waliokosa nafasi za uongozi kushirikiana na viongozi waliochaguliwa ili kudumisha amani na maendeleo ya taifa.
Dk. Gaville pia aliwakumbusha Watanzania juu ya changamoto za hali ya hewa, akiwataka wakulima kutumia mbegu zinazostahimili ukame na wananchi wote kutunza vipato vyao badala ya kuendekeza matumizi yasiyo ya lazima.
Mgeni maalum katika ibada hiyo, Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Iringa, aliwahimiza waumini kuishi kwa mujibu wa maandiko matakatifu ili kukabiliana na changamoto za kidunia.
Alisema kila mtu anapochukua nafasi yake kikamilifu katika familia na jamii, matatizo mengi yanayowakabili vijana kama ukatili wa kijinsia na mmomonyoko wa maadili yanaweza kuepukwa.
Askofu Mstaafu wa KKKT Dayosisi ya Iringa, Prof. Owdenburg Mdegella, alizungumzia changamoto za kijamii zinazoukabili mkoa wa Iringa, zikiwamo matendo ya ukatili, udumavu na maambukizi ya UKIMWI.
Alisisitiza kuwa wazazi wana jukumu la kukemea na kuripoti vitendo vya ukatili dhidi ya watoto badala ya kuficha wahalifu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED