Fundi saa aliyetikisa jiji akihudumia vigogo, mageuzi teknolojia yamgeuza ‘choka mbaya’

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:01 PM Dec 27 2024
Fundi saa aliyetikisa jiji akihudumia vigogo, mageuzi teknolojia yamgeuza ‘choka mbaya’
Picha:Mtandao
Fundi saa aliyetikisa jiji akihudumia vigogo, mageuzi teknolojia yamgeuza ‘choka mbaya’

KATIKA jiji la Abuja, nchini Nigeria, kuna duka la kutengeneza saa la Bala Muhammad. Hapo kuna fundi saa maarufu anayejulikana kwa jina, Baba Bala.

Katika zama hizo teknolojia haijakua, alikuwa maarufu maradufu, huku mwenyewe ‘akikusanya’ pesa ndani na nje ya mipaka kwa ufundi wake huo.

Duka hilo liko katikati ya barabara kuu ya Kaduna, jijini Abuja, mtaa maarufu uliojaa maduka ya vifaa vya ujenzi na ndani yake kulikuwa na saa nyingi zilizozunguka kila kona, kila moja ikionesha muda wake. 

Hapo fundi huyo, ambaye sasa ana umri miaka 68, ametulia kwenye kiti kidogo kilichozungushwa na meza yake ya kazi.

Baba Bala, alikumbuka enzi zilizopita alipokuwa akitengeneza saa kwa haraka, wakati aliokubaliana na wateja wengi waliokuwa wanamletea saa zao kurekebishwa. 

"Kuna wakati nilikuwa napokea zaidi ya saa 100 kwa siku moja," anaelezea, akionesha jinsi biashara yake ilivyokuwa na umaarufu mkubwa.

Anasema,  leo, anakumbwa na wasiwasi mkubwa akitamka kwa kulalamika: “Teknolojia mpya, hasa simu za mkononi, zinauwa biashara yangu." 

Mzee huyo anakiri kazi aliyojivunia kwa miaka mingi ilikuwa ikielekea ukingoni na kwamba maarifa aliyopata kutoka kwa baba yake na nduguye mdogo, yanaanza kupotea umuhimu wake.

Baba Bala anaeleza jinsi alivyofikia hatua hiyo, baada ya kufundishwa na baba yake, Abdullahi Bala Isa, aliyejulikana fundi wa saa maarufu katika miji mingi ya nchi za Afrika Magharibi.

Baba yake Bala, ana historia ya kusafiri maeneo kadhaa Magharibi mwa Afrika kwa zaidi ya miezi sita kuanzia, Senegal hadi Sierra Leone, kwenda kufanya kazi moja; kutengeneza saa za watu zilizoharibika.

Kuna wakati Baba Bala alikuwa akiishi jiji kuu la Nigeria, wazito na wanasiasa wa mahali alikoishi, alikuwa fundi wao akiwatengenezea saa zao na daima ‘hakulala’ akitajwa kuwa na kipato kinachojitosheleza.

Ana simulizi ya kukumbuka maofisa wakuu wa serikali, walikuwa wakimletea saa zao za mikononi aina ya Rolex zenye thamani ya Dola za Marekani 10,000 (sawa na Sh. milioni  24).

Anasema, saa aina hizo huwa zinapendeza na ndio maana anavutiwa zikiitwa ‘saa  kutoka Uswisi’, yeye naye ‘hajambo’ mkononi akiwa na saa nyingine kutoka Uswisi aina ya Longines, akihusudu hata analala nayo.

"Nikitoka nyumbani kwangu nikumbuke sijavaa saa yangu, hunibidi nirejee nyumbani. Hakika siwezi kukaa bila saa yangu - ina umuhimu kwangu," anaeleza fundi Bala

BABA KAMA MWANA

Katika duka lake amening'inizia picha kubwa ya baba yake,Abdullahi Bala Isa, aliyopigwa akiwa ofisini mwake kabla ya kifo chake mwaka 1988.

Marehemu Mzee Isa, anajulikana sana kwa umahiri wa kurekebisha saa zilizoharibika katika maeneo mengi kama vile Freetown, Sierra Leone na Dakar, Senegal, hakushindwa  hata vile vilivyoshindikana,akitatua na kuna wakati alikuta mrundikano wa saa.

Baba Bala, anasema wote hawajui baba yao alikotoa ujuzi wa kutibu saa mbovu, kukiwa na tetesi aliunasa enzi za ukoloni wa Muingereza, nchini mwao. 

Fundi Bala akiwa mzaliwa wa miaka minne kabla ya Nigeria kupata uhuru mwaka 1960, ana nyongeza baba yake katika simulizi:

"Babangu alikuwa mtaalam wa kutengeneza saa na alikuwa akisafiri maeneo mengi kuunda saa. Alijifunza nikiwa mdogo na nikaamua kufuata nyayo zake nilipoinukia ukubwani.”

"Mimi nilianza kuwa fundi wa saa nilipokuwa na umri wa miaka kumi," anakumbuka Baba Bala, akieleza jinsi alivyovutiwa na taaluma ya saa tangu utotoni.

KUTOKA SHULE

Anajigamba: "Wakati wenzangu walikuwa wanalia kwa kutokuwa na pesa, mimi nilikuwa na pesa kwa sababu nilikuwa nikifanya kazi."

Anasema ni umahiri uliomvutia hata mwalimu wake akiwa shuleni, akiwa na simulizi: 'Mwalimu alikuwa na saa ambazo zimeharibika.

“Alikuwa amejaribu kuzipeleka kwa fundi zitengenezwe. Lakini haikuwezekana, aliponijulisha hayo, alinipatia saa zake na nikamtengenezea siku hiyo hiyo.''

Fundi huyo anaeleza, saa zilikuwa zikitambulika kama mavazi ya kila siku -  ilikuwa ni vigumu kuona mwanaume ambaye hajavaa saa ya mkononi.

Watu wengi walikuwa wakileta saa zao zitengenezwe na baadhi yao hawarudi kuzichukua. Maisha ya Baba Bala yalianza kubadilika, kama ilivyokuwa kwa wateja wengi wa zamani.

"Leo, vijana wanatumia simu kutafuta majibu badala ya saa," anaeleza wakati ambao biashara yake ilijulikana na kwa matajiri na viongozi wa kiserikali.

Analalamika sasa ni vigumu kupata wateja wapya, akitamka kwamba "saa za kisasa zinageuza kila kitu."

Mtaani hapo anakopatikana anasema, maduka ya saa eneo la Kaduna, maduka mengi yamefungwa na baadhi ya marafiki zake wameshajiuzulu au wamefariki.

Lakini Fundi Isa Sani (65), mfanyabiashra mwezake naye bado anaendelea na biashara ya kutengeneza  saa zilizoharibika .

'Nikienda dukani kwangu kila siku, hukaa bila kupata mteja yoyote siku nzima, lakini bado sijakata tamaa tangu mwaka 2019,'' anasema.

''Nina shamba ambalo watoto wangu hunisaidia kulima na tunajikimu kimaisha kupitia mavuno ya shambani,'' anasema.

Kwa unyonge, anasema: ''sifikirii kuwa kurekebisha saa zilizoharibika itakuwa biashara ya kunoga kama awali.'' 

WADAU MTAANI

Vijana wa eneo hilo, kama Faisal Abdulkarim na Yusuf Yusha'u walio na umri wa miaka 18, wanakubali kwamba siku hizi, simu za mkononi zimechukua nafasi ya saa.

"Nikiangalia simu yangu, naweza kujua muda kwa urahisi,"anasema mmoja wao.

Dk. Umar Abdulmajid, Mhadhiri wa Chuo cha Mawasiliano cha Yusuf Maitama anaamini mambo yatabadilika, akiwa na kauli:

''Saa za zamani hazipo tena kwa hivyo, hakuna shughuli ya kuzirekebisha, lakini kuna saa zinazotumia intaneti zimeanza kuingia kwahivyo zitahitaji fundi wa kuzitengeza zikiharibika.''

Baba Bala anakubali mabadiliko hayo, lakini akijua anapitia changamoto kubwa.

"Simu na teknolojia ya kisasa vinafifisha biashara yangu, lakini mimi bado nipo hapa na nitaendelea kutoa huduma," anasema, akieleza kuwa biashara yake inahitaji kubadilika ili kuendana na wakati.

Baba Bala hutumia muda mwingi katika duka lake akisikiliza habari kwa njia ya redio

"Watu wengi wamekuwa wakileta saa zao zitengenezwe na baadhi yao hawarudi kuzichukua zimejaa hapa,'' anasema Baba Bala.

Lakini Baba Bala amekataa kufunga duka lake,- mtoto wake wa kike ambaye huuza nguo na humnunulia kadi za simu, angalau auze apate kipato cha siku.

Hata hivyo, anajivunia kuona mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 12 akitaka kuwa rubani, na alifurahi kuona familia yake inavyoendelea kuona dunia kwa mtazamo tofauti.