DC awapa mbinu wananchi za kukacha mikopo ‘kausha damu'

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:28 AM Dec 28 2024
MKUU wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele.
Picha: Mtandao
MKUU wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele.

MKUU wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele, amewataka wananchi wilayani hapa kujiweka kando na mikopo umiza maarufu kama 'kausha damu' kwa kutumia taasisi za fedha zinazotambuliwa zikiwamo benki kupata mikopo iliyodhibitiwa viwango vya riba na masharti.

Amesema benki zote na taasisi za fedha halali zinazotoa huduma katika wilaya hiyo zimeweka masharti nafuu ikiwamo kutoa riba nafuu kuruhusu wananchi wengi kuachana na mikopo umiza inayodidimiza uchumi wao. 

Gowele alitoa wito huo wakati akifungua tawi jipya la benki ya CRDB katika mji wa mpakani, Sirari, na kukemea tabia ya baadhi ya taasisi kutoa na kuweka fedha kutoza wananchi riba zaidi ya asilimia 50. 

Alisema serikali inashirikiana na taasisi za kifedha zikiwamo benki zote ili wajasiriamali wadogo ambao hawajafikia vigezo vya kukopa fedha nyingi kupata uwezeshaji kupitia mikopo ya kawaida ili kuwanusuru na mikopo yenye masharti magumu inayowarudisha nyuma kimaendeleo na kimaisha. 

 "Ni rai yangu kwamba wananchi kutoka makundi yanayopendelewa ya wanawake, vijana na walemavu watarejesha fedha wanazokopa kwa wakati ili zirejee katika mzunguko na kuwezesha wengine kukopa kwa urahisi, "alisema. 

Uwapo  wa taasisi hizo karibu na wananchi, alisema  zimewezesha kufanyika malipo kwa njia za kidijitali na ulipaji kodi na tozo za serikali kwa ajili ya huduma mbalimbali ikiwemo umeme na maji na serikali kukusanya mapato. 

Meja Gowele alizitaka benki wilayani Tarime kubuni mipango ya kutoa elimu kwa umma kuhusu utunzaji akiba na ujasiriamali kuhakikisha fedha zao zinakuwa salama na kuongeza nidhamu katika matumizi. 

Ofisa Mkuu Usimamizi Biashara wa CRDB, Boma Raballa, alisema hivi sasa benki hiyo inaendesha mpango wa kuuza hati fungani za miundombinu ya Samia ili kuwezesha kujenga miundombinu ya barabara. 

Alisema kiasi cha uwekezaji kinaanzia Sh.500,000 na hakina kikomo cha juu cha uwekezaji na mwekezaji atapewa faida ya asilimia 12 kila robo ya mwaka na haitakuwa na kodi ya zuio. 

"Tunawashauri wananchi wote waliowekeza katika hati fungani hiyo watumie fursa hiyo kama dhamana ya kupata mkopo katika benki au taasisi yoyote inayotambulika hapa nchni kwa kuwa inawezekana," alisema. 

·    Imeandaliwa na Ambrose Waitangwa, Samson Chacha (TARIME)