Biteko kuwahakikishia wananchi wa Ijinga, Magu huduma ya umeme

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 04:57 PM Dec 24 2024
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.
Picha:Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amewahakikishia wakazi wa Kijiji cha Ijinga, wilayani Magu, kupata huduma ya umeme.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Magu, Dk. Biteko amesema kijiji hicho, kilichopo kwenye kisiwa, ni pekee kilichobaki bila umeme wilayani humo. Serikali imetenga Sh. milioni 619 kwa ajili ya kufikisha umeme wa jua (solar), na mkandarasi kutoka Kampuni ya Master Volt Ltd tayari yupo eneo la mradi.

Mbunge wa Magu, Boniventura Kiswaga, amesema asilimia 99 ya vijiji wilayani humo vina umeme, akishukuru juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, hususan katika kusambaza majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50 ili kuokoa mazingira na afya za wananchi.

Msimamizi wa Miradi Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Awesa Rashid, amesema REA inaendelea kusambaza umeme kwenye vitongoji 15 kwa kila jimbo, huku wananchi wakihimizwa kuchangamkia kuunganishwa umeme kwa Sh. 27,000 tu.

Pia, REA inaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi za kupikia, kwa mujibu wa mkakati wa taifa wa Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034. Mkoa wa Mwanza utasambaziwa majiko 19,530 kwa bei ya ruzuku.

Sebastian Boniphace, mkazi wa Magu, amesifu mpango huo wa serikali, akisema utapunguza ukataji miti na athari za mkaa na kuni.