KRISMASI, MWAKA MPYA: Ujumbe wa Bagonza kwa wanasiasa, matajiri

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:54 AM Dec 24 2024
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza.
Picha:Mpigapicha Wetu
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza.

ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza katika salamu zake za Krismasi na Mwaka Mpya 2025, ametoa ujumbe maalumu kwa matajiri na wanasiasa.

Katika salama zake hizo, Askofu Bagonza anasifika kwa kutoa maandiko yaliyojaa fikra tunduizi, anatoa wito kwa jamii, hasa matajiri "kuwageukia waliowasababishia utajiri wao ili nao wanufaike".

Kwa viongozi wa kisiasa, Askofu Bagonza ana ujumbe maalumu kwa aliowaita "viongozi wa kisiasa ambao hupatikana kwa kupigiwa kura", akisema "wapigakura maskini ndio huwatengeneza viongozi matajiri, ingawa wao husalia na umaskini".

Askofu Bagonza anasema katika andishi lake hilo: "...Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu; ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake (ananukuu kitabu cha 2Kor 8:9 katika Biblia).

"Habari za maskini kutajirisha matajiri si ngeni kwetu. Tumewaona wakulima maskini wakitajirisha matajiri, waumini maskini wakiwatajirisha wahubiri. Bodaboda maskini wakiwatajirisha wauza pikipiki na maaskari barabarani.

"Wapigakura maskini wakitengeneza viongozi matajiri. Lakini maskini hawa hatuwezi kuwaita kuwa ni Yesu Kristo."

Askofu Bagonza anasema matajiri hawaonekani kuwatajirisha maskini. Badala yake kinachoonekana ni matajiri wanaodhani wana bidii na akili na maskini kuambiwa ni wavivu na hawana akili.

"Kwao hawa matajiri, kutajirika ni akili na ujanja. Hawa matajiri huwaona maskini kuwa ni wavivu na wasio na akili. Ukweli ni kwamba, utajiri na umaskini vina uhusiano wa karibu sana na mara nyingi uhusiano huu umejengwa katika unyonyaji.

"Kuzaliwa kwa Yesu kulileta picha tofauti. Yeye alikuwa tajiri, ili maskini wawe matajiri na alizaliwa katika hali ya umaskini, ili sisi tuwe matajiri. Maskini na matajiri wote wana nafasi katika kuzaliwa kwa Yesu.

"Lakini kwa namna ya pekee, Yesu alizaliwa kwa ajili ya waliokosa tumaini na kukosa mtetezi. Jamii yetu inalo la kujifunza kutoka Yesu Kristo. Tunaalikwa kumtazama Yesu katika sura ya watu wanateseka."

Askofu Bagonza anataka watu wamtazame Yesu katika sura ya Mpalestina anayeteketezwa na mabomu ya nchi tajiri. Wamtazame Yesu kama mtu wa Ukraine anayekaangwa kwa mabomu ya Russia.

"Mtazame Yesu kama mwanaharakati anayepigania haki za kidemokrasia, anayetekwa na kupotezwa kama gaidi. Mtazame Yesu kama mtu maskini anayelazimika kununua haki zake katika ofisi za umma.

"Mtazame Yesu kama mwananchi maskini anayelazimika kununua uponyaji na wokovu wake. Mtazame Yesu kama mtu asiye mwanachama wa chama chochote anayepoteza haki ya kuchaguliwa kuwa kiongozi na kuishia kuwachagua wengine wamwongoze.

"Na haya yanapotokea, mtazame Yesu katika sura ya jamii inayokosa haki wakati watu wote wako kimya. Kwa umaskini wake na utajiri wake, Yesu Kristo amezaliwa kwetu. Yeye ni mtawala wa haki. 

"Kwake hakuna mizengwe wala hila. Anatualika sote tumpokee na kumpeleka nyumbani kwetu, ofisini kwetu na kila mahali. Ninawatakia Noel njema na Mwaka Mpya wa 2025," Askofu Bagonza anahitimisha andishi lake la salamu za Krismasi na Mwaka Mpya.

ASKOFU MWAMAKULA

Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania na Afrika Mashariki, Emmaus Mwamakula katika ujumbe wake wa Krismasi na Mwaka Mpya, amegusia masuala ya utekaji, ukosefu wa ajira na kupanda kwa gharama za maisha.

"Tunaingia katika kusherehekea Sikukuu ya Krismasi wakati watu wetu wengi wapo katika hali ya shaka, hofu, hata kukata tamaa kwa mambo mengi sana," anasema.

Askofu huyo anasema hali ya usalama kwa maisha ya watu na mali zao imezorota kwa kiasi kikubwa, vitendo vya utekaji na mauaji vimeweka jamii ya watanzania katika taharuki.

"Vijana wetu kadhaa waliotekwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita hawajulikani waliko. Pia, hali ya usalama wa majengo nchini inaogopesha, moto unaunguza majengo huku mengine yakiporomoka na uwezo wa uokozi ni mdogo sana," anasema.

Askofu Mwamakula anasema ukosefu wa ajira nchini umekuwa janga linalotishia ustawi wa vijana. 

Anasema uhalifu wa kisiasa unaonekana kuhalalishwa na watu wenye mamlaka kiasi cha kusababisha hata kufanyika mambo yasiyo ya uhalali katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka huu.

Askofu Mwamamkula pia amezungumzia ubora wa elimu kwa shule za serikali, akisema hauridhishi na kutaka juhudi zaidi ziongezwe ili kuzifanya ziwe bora zaidi.