Washangaa watuhumiwa ukatili kuwa uraiani

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 12:15 PM Dec 24 2024
Mkurugenzi wa Taasisi ya Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI), Janeth Mawinza.
Photo: Together for Girls/Alexandra Tucci Thomas/Tanzania.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI), Janeth Mawinza.

WANAHARAKATI wanaopinga unyanyasaji wa kijinsia, ukatili na rushwa ya ngono nchini wamesema licha ya kutumia muda na nguvu kubwa katika kukemea vitendo hivyo na hata kuwapeleka mahakamani watuhumiwa, wamekuwa wakishangazwa kuwaona wahusika wakitamba mitaani baada ya kesi kuisha.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI), Janeth Mawinza, alisema juzi kuwa moja ya mambo yanayowakatisha tamaa na kuwarudisha nyuma ni kuona kesi za vitendo vya ukatili zikishindwa kumalizika katika hatua nzuri.

Alisema wamekuwa wakifuatilia kesi mbalimbali kwa kushirikiana na wadau kwa kufuata taratibu zote za kisheria, lakini kesi hizo zimekuwa hazifiki mwisho unaoridhisha, jambo ambalo linaweza kuhatarisha jamii na kutowatendea haki waathirika.

"Tunafuatilia kesi mbalimbali japo umalizikaji umekuwa changamoto, kuna ambazo zinaisha lakini inaumiza pale ambapo uamuzi umefanyika, mtoto aliyetendwa vitendo vya ukatili ameshinda, lakini mhusika yuko nje, hilo kwetu tunaona ni tatizo kubwa.

"Sisi tunafuatilia tunampeleka mtuhumiwa mahakamani na ameonekana kuwa ana hatia, anatakiwa kwenda jela, aidha miaka 30 au kifungo cha maisha, lakini tunajiuliza kwanini anabaki nje? Tunatengeneza nini? Tunajiaminisha vipi kwamba hatawadhuru wengine?

"Tunategemea kwamba wanaokutwa na hatia wanapopelekwa gerezani wanakwenda kupata mafunzo ya kumfanya akirudi uraiani asifanye tena hivyo vitendo, sasa kama anabaki uraiani inaleta picha gani? Hadi sasa tumeona kesi mbili ambazo mtuhumiwa anahukumiwa lakini anabaki nje," alisema Janeth.

Alisema kuwa kila wanapojaribu kufuatilia, wahusika hao wamekuwa wakihama maeneo mbalimbali ili kujificha licha ya kwamba hukumu zao zilishatolewa. Kutokana na ushirikiano wanaopata kutoka kwa jamii, inawasaidia kupata taarifa za mienendo ya wahusika hao wa vitendo vya ukatili.

"Jamii sasa imeshafunguka, wanajamii wanavunja ukimya lakini huku kwenye umalizikaji mnyororo hauunganiki vizuri, unakatikakatika, shida iko wapi? Kutokana na hali hii tulienda kutoa taarifa Ustawi Halmashauri ya Kinondoni tukakabidhiwa kwa afande lakini kuzungushwa kulikuwa kwingi.

"Pamoja na kufanya kazi kwetu kuamsha jamii iseme, lakini kuna mahali wanarudishwa nyuma, leo nikiona huyu kaenda hakuna kilichofanyika, tunawafanya watu wanyamaze lakini tunaendelea kupaza sauti kupitia vyombo vya habari ili mamlaka isikie," alisema Janeth.

Mjumbe wa WAJIKI, Hancy Obote, alisema wale ambao ni wakosaji wanawaona wao kama maadui wakubwa, hata kuwanyooshea vidole na wakati mwingine wanawatishia, mazingira ambayo yalisababisha kipindi fulani mkurugenzi wao apelekwe kukaa mahali salama.

Alisema hali hiyo inawapa shida na kusababisha wakati mwingine kufikiria kukata tamaa.

"Jambo lingine ni kwa wenzetu wenye mamlaka ambao sisi tunasema tunafanya uchechemuzi lakini watendaji ni wao, japo wakati mwingine wanaleta kujuana, rushwa na ubabe.

"Mwisho wa siku anayetumia nguvu nyingi na kuumia ni wewe, lakini wao maisha yanaendelea, kwa sababu tunapambana kesi zinakwenda mahakamani lakini zinaisha mtuhumiwa anaonekana mtaani, hata jamii inakosa imani, wanaona ni yaleyale, hapa tunatengeneza bomu, mazingira haya yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani," alisema Obote.

Mkurugenzi wa WAJIKI, Janeth, alitoa tahadhari kuwa vyombo vya uamuzi visiposimama na kuwasaidia walalamikaji, vitakuwa wanafanya kitu cha hatari kwa kuwa watanyamazisha sauti za jamii.