Ajali yakatisha uhai wa Mkurugenzi Hazina

By Joyce Lameck , Nipashe
Published at 12:04 PM Dec 24 2024
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Msajili wa Hazina, Amos Nnko.
Picha:Mtandao
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Msajili wa Hazina, Amos Nnko.

MATUKIO ya ajali mwishoni mwa mwaka yameendelea kuacha vilio na majonzi katika jamii baada ya juzi aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Msajili wa Hazina, Amos Nnko, kufariki dunia kwa ajali ya gari.

Nnko amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea Desemba 22 huko Same, mkoani Kilimanjaro. Katika ajali hiyo, binti yake wa kwanza, Maureen Nnko naye alifariki dunia.

Taarifa iliyotolewa jana na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu ilieleza" "Msajili wa Hazina anasikitika kutangaza kifo cha Amos Nnko aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kilichosababishwa na ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Same, mkoani Kilimanjaro."

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa mke wa marehemu, Agnes Nnko na watoto wao Marilyn, Melvin na mwanafamilia mwingine aitwaye Sylvana, wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) na Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi).

Ilielezwa katika taarifa hiyo kuwa mipango ya mazishi inaendelea kuratibiwa na familia ya marehemu kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Hivi karibuni kumekuwa na mfululizo wa matukio ya ajali za barabarani ambazo zimesababisha vifo vya watanzania wengi.

Desemba 18, mwaka huu, huko Mikese, mkoani Morogoro, gari aina ya Coaster liligongana na lori la mizigo na kusababisha vifo vya watu 15 na kujeruhi saba. Baadaye mmoja wa majeruhi hao alifariki dunia wakati anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kufanya idadi ya vifo kuwa vya watu 16. 

Juzi katika kijiji cha Kabukome, Kata ya Nyarubungo, wilayani Biharamulo, basi la kampuni ya Capro One lenye namba za usajili T857 DHW lilifeli breki katika mteremko na kurudi nyuma kisha kupinduka na kusababisha vifo vya watu 11 na wengine 16 kujeruhiwa.

Kutokana na matukio hayo, Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza Jeshi la Polisi kuwa na mfumo wa leseni za udereva utakaowapunguzia alama madereva wanaofanya makosa yenye kuhatarisha usalama na uhai barabarani.