VYAMA vya Msingi vya Ushirika (AMCOS), vinavyolima zao la tumbaku katika halmashauri ya Ushetu, mkoani Shinyanga, vimebuni mbinu mpya ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo, kwa kutoa motisha ya bodaboda na baiskeli kwa wakulima.
Mwenyeki wa Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU), Emmanuel Nyambi, aliyabainisha haya jana wakati akizungumza na vyombo vya habari, akisema lengo ni kuzalisha zaidi na kufikia lengo la makusanyo waliyojiwekea kila msimu.
Alisema namna walivyojipanga na kuhakikisha wanafikia lengo la kuzalisha kilo milioni 17 za tumbaku walizoingia mkataba na makampuni yanayonunua zao hilo.
Alisema Chama cha Msingi Ngokolo, kimebuni mbinu mpya ya kuhakikisha wanafikia lengo la kilo walizoingia mkataba na wanunuzi, kwa kutoa motisha ya pikipiki na baiskeli kwa wakulima wake wanaozalisha zaidi.
Nyambi alisema, fedha zinazonunua motisha hizo zinatokana na ushuru wanaowatoza wakulima wake na kurejesha kwao, kwa kuwanunulia pikipiki pamoja na baiskeli na kuvitaka vyama vingine kuinga mbinu hiyo, ili kuongeza uzalishaji katika zao la pamba na tumbaku ambayo ndio chanzo kikuu za mapato ya Ushetu.
Alisema, msimu wa kilimo 2024/2025 walifanya vema katika uzalishaji na kuchangia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Ushetu Sh. bilioni 65.987 na msimu ujao wanatarajia kuchangia zaidi kutokana na motisha iliyoibuliwa na vyama vya msingi na kuwasihi kuendelea kuzingatia maelekezo wanayopewa na maofisa kilimo.
Aliwataka viongozi vyama hivyo kubuni miradi ya kimaendeleo katika vyama vyao, ili kuondokana na kutegemea ushuru pekee wa tumbaku, pamba na itawasaidia kujiendesha katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
“Sikukuu hizi za Krismas na mwaka mpya, ziwafanye wakulima wangu wakatelekeza mashamba yao ya tumbaku na kuja kuyatembelea, baada ya mwaka mpya, tutakuwa tumekwama kufikia malengo ya kilo milioni 17 tukumbuke mashamba na kupeleka watoto shule mwakani,” alisisitiza Nyambi.
Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Uyogo, Maganga Masanja, alikipongeza chama cha Chongolo, kwa kutoa pikipiki na baiskeli kwa baadhi ya wakulima wake waliofanya vema kwenye uzalishaji wa zao la tumbaku na yeye anajiandaa kutoa zawadi kwa watakaofanya vema kwani ni haki yao kupewa kwa sababu ushuru unatoka kwao.
Mmoja wa wakulima wa tumbaku, Kulwa Shoto, alisema sababu nyingine inayowafanya wazalishe zaidi ni kutokana na bei kupanda kila mwaka kutoka dola 1.55 mwaka 2020 hadi kufikia wastani wa dola 2.38 mwaka 2024.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED