Waombwa 'kupiga kambi' ndani ya jamii kutoa elimu ya kisheria

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 03:01 PM Dec 24 2024
Innocent Masanja akijitambulisha
Picha: Sabato Kasika
Innocent Masanja akijitambulisha

WATUMISHI wa Dawati la Msaada wa Kisheria wa Jiji la Dar es Salaam, wameombwa kutenga muda wa kukutana na viongozi wa ngazi za na kuwapa elimu ili kuwajengea uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria.

Ombi hilo limetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Kituo cha Sauti ya Jamii Kipunguni, Seleman Bishagazi kwa watumishi hao walipofika kituoni hapo kujitambulisha ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao kutoa elimu itakayosaidia jamii kujua   
haki zao za Kisheria.

Bishagazi alisema katika ngazi za chini kuna migogoro mingi ikiwamo ya ardhi, mirathi, ndoa na ukatili wa kijinsia, na kwamba watumishi hao hawana budi kushuka chini hadi kwa viongozi wa ngazi za chini kuwapa elimu.

"Tuna viongozi wa mabaraza  ya ardhi ya kata wanapelekewa migogoro ya ardhi hawajui Sheria inakuwa vigumu kuitatua," alisema Bishagazi.

Aliongeza kuwa hata viongozi wa serikali za mitaa nao wanapaswa kupata elimu ya mambo ya kisheria ili nao wasaidie wananchi wanapofika kwao.

Farida Mwishehe akitoa maoni.
"Huku chini Kuna migogoro mingi, hivyo ninaomba mtenge muda muandae ratiba ya kuja kuwapa elimu ya Sheria angalau viongozi wawe na uelewa wa kutatua migogoro au kuwaelekeza wananchi waende wapi wapoluwa na tatizo fulani," alisema.

Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Dawati la Msaada wa Kisheria Jiji la Dar es Salaam, Innocent Masanja, yeye na wenzake watalifanyia kazi ombi hilo.

Amekiri kuwa Kuna changamoto nyingi kwenye jamii ambazo nyingine zinatokana na kutoelewa sheria na kusababisha kuwapo kwa migogoro mingi isiyoisha.

"Tulichokuja kufanya ni sehemu ya kampeni iitwayo Mama Samia Legal Aid inayolengwa kuwezesha wanajamii kujua haki zao za kisheria, hivyo tutaendelea kushirikiana nanyi na tutafanyia kazi ombi na ushauri wa mkurugenzi," alisema Masanja.

Mmoja washiriki wa wanufaika wa elimu hiyo, Farida Mwishehe alisema ana changamoto nyingi ambazo zimekwamisha mambo mengi ya kifamilia, na kwamba anaamini kupitia wataalam hao wa Sheria atawafikishia kero zake ili apate ushauri wa jinsi ya kuzitatua.

Baadhi ya wananchi wakiwasiliza watumishi hao.