Bashungwa asisitiza amani, upendo, umoja

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 10:41 AM Dec 27 2024
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa.
Picha:Mtandao
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, ameomba Watanzania kuendelea kutunza tunu za upendo, umoja, amani na kufanya matendo ya huruma.

Bashungwa alitoa kauli hiyo juzi alipoungana na waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Kiruma katika ibada ya Krismasi.

Waziri Bashungwa alisema serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini katika kufundisha wananchi kuishi kwa upendo na amani.

“Tukipendana tutakuwa wamoja, tutakuwa na amani, na tutadumisha tunu zetu ikiwamo ya ujirani mwema na kufanya matendo ya huruma,” alisema.

Awali, Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kiruma, Padre Salapion Mberwa, aliwahimiza waumini wa kanisa hilo, kudumisha upendo na amani.

“Mahali penye upendo kuna umoja. Tusherehekee sikukuu hii  kwa kuenzi upendo na umoja kwa sababu mahali penye umoja ndipo penye amani,”alisema Padre Mberwa.

Juzi katika sehemu ya salamu zake za Sikukuu ya Krismasi, Rais Samia Suluhu Hassan, aliwakumbusha Watanzania juu ya upendo kwa ndugu na jirani, juu ya uzalendo kwa taifa na kuishi katika kweli.

Kadhalika, aliwakumbusha juu ya unyenyekevu hasa wanapojaliwa nafasi za kuwatumikia wengine, kuwa na shukrani ikiwamo kuungana kwa pamoja kuiombea nchi ili iendelee kudumu katika amani, umoja na utulivu.

Rais Samia aliwataka kusherehekea sikukuu hiyo kwa kujumuika na familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa furaha na upendo na kutaka historia ya Yesu Kristo iwape tafakari juu ya mwanzo mpya katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.