CAF yaibeba Simba Tunisia

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 03:45 PM Dec 27 2024
CAF yaibeba Simba Tunisia
Picha:Mtandao
CAF yaibeba Simba Tunisia

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limetangaza kuifungia CS Sfaxien ya Tunisia kucheza mechi zake mbili za mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho bila mashabiki kufuatia vurugu walizofanya dhidi ya CS Constantine ya Algeria.

Katika mechi hiyo CS Sfaxien ikiwa mwenyeji ilifungwa bao 1-0, mashabiki wao walitupa mafataki, jambo ambalo limepigwa marufuku na wasimamizi hao wa soka Afrika.

CAF pia imewatoza CS Sfaxien faini ya Dola za Marekani 50,000 (sawa na Sh. milioni 119).

Adhabu hiyo ya CS Sfaxien, itainufaisha Simba ambayo itasafiri kwenda Tunisia kucheza mchezo wa raundi ya nne dhidi ya timu hiyo, mechi itakayofanyika Januari 5, mwakani.

Mechi nyingine ambayo CS Sfaxien itacheza bila mashabiki wake ni Januari 19, mwakani pale itakapowakaribisha Bravos do Maquis ya Angola.

Hata hivyo, timu hiyo huenda ikakumbana na adhabu nyingine  kutokana na vurugu zilizotokea katika mechi dhidi ya Simba iliyochezwa Desemba 15, mwaka huu  kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, wenyeji wakishinda mabao 2-1.

Mashabiki na wachezaji wa CS Sfaxien  walifanya vurugu katika mechi hiyo kufuatia mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis, kufunga bao dakika za 'jioni'.

Baada ya bao hilo lililoipa Simba ushindi kufungwa, kulitokea vurumai kubwa ndani ya uwanja, ambapo benchi la ufundi na baadhi ya wachezaji walimvamia mwamuzi wa mchezo, huku jukwaani nako kukiwa na tafrani kati ya mashabiki wa timu hiyo pamoja na wenyeji  na kupelekea uharibifu wa viti kung'olewa.

Watunisia hao waliondoka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa huku wakiahidi watalipa kisasi watakapokuwa nyumbani kwao.

Kucheza bila mashabiki inaonekana ni faraja kwa Simba kwa sababu pamoja na itakuwa imelainishiwa mchezo kutokana na wenyeji kukosa faida ya kushangiliwa ili kuwaongezea hamasa wachezaji wao.

Wakati hayo yakiendelea, Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, ameweka wazi kikosi chao kitaongezewa nguvu ya  wachezaji wapya kipindi cha dirisha dogo la usajili kwa ajili ya kukiimarisha.

Mangungu alisema uongozi unaendelea kukamilisha mazungumzo na baadhi ya wachezaji inaowahitaji ili kuifanya Simba iwe na nguvu zaidi katika michuano ya kimataifa na Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Ni kweli tunatarajia kuongeza wachezaji, kwa tathimini ya kocha kuna mahitaji, tumeashaanza kuzungumza na baadhi ya wachezaji wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kujiunga na timu yetu, mambo yatakapokuwa tayari tutawatangazia," alisema Mangungu.

Tayari Simba imeshakamilisha usajili wa winga, Elie Mpanzu, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo), ambaye tayari ameshaanza kutumika kwenye mechi za Ligi Kuu Bara.

Wakati huo huo, kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka leo jijini ili kuelekea Singida kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida Black Stars utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa CCM Liti mkoani humo.

Simba yenye pointi 37 ndio vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara watakutana na Singida Black Stars ambayo ina pointi 33 iko nafasi ya nne katika msimamo imekuwa na msimu mzuri.

Nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo inashikiliwa na Yanga yenye pointi 36 ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 33, lakini ina uwiano mzuri wa magoli ya kufunga na kufungwa ukilinganisha na Singida Black Stars.