Ramovic aanika siri ya ushindi Yanga SC

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 03:48 PM Dec 27 2024
 Sead Ramovic.
Picha:Mtandao
Sead Ramovic.

KOCHA Mkuu wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, Sead Ramovic, ametaja sababu inayowapa ushindi timu yake ni kufuatia wachezaji wake kucheza kwa kuzuia na kushambulia pamoja bila kutegeana katika mechi zao za hivi karibuni.

Ramovic ametoa kauli hiyo baada ya kupata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Dodoma Jiji katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa juzi.

Kocha huyo alisema hali hiyo inasaidia kuondoka na pointi tatu muhimu lakini pia akiwaambia wanachama na mashabiki wa timu hiyo watafurahi zaidi pale wachezaji wake watakapokuwa na utimamu wa mwili kwa asilimia 100.

Alisema kwa sasa kikosi chake kinamudu zaidi kucheza mfumo anaotaka kipindi cha kwanza tu kwa sababu bado wachezaji hawajakuwa fiti kwa kiwango cha kutosha.

"Katika mfumo wangu nataka kila mchezaji akimbie, azuie wakati timu haina mpira na kushambulia wakati tuna mpira, tunazuia pamoja na tunashambulia pamoja.

Ukiangalia tumecheza michezo mitatu ndani ya siku saba, kwa hiyo wachezaji wangu wanatumia kipindi kimoja kuamua mechi, kama ukifuatilia utagundua tunafunga mabao mengi kipindi cha kwanza ambacho tunacheza kwa kasi na kufanya kama ninavyohitaji, hatufanyi hivyo kipindi cha pili kwa sababu tayari wanakuwa wameshachoka.

Lakini kwa bahati nzuri wana uwezo wa kuhimili mashambulizi, nadhani tunakwenda taratibu, tutaanza kucheza kwa kasi kwa dakika 90, mambo haya yatakuja hatua kwa hatua," alisema kocha huyo raia wa Ujerumani.

Hata hivyo aliisifia Dodoma Jiji akisema ni timu nzuri, yenye wachezaji wenye nguvu, waliokuwa wakishambulia kwa kushtukiza na kuwapa 'tabu' wakati fulani.

Mabao ya Yanga katika mchezo huo wa juzi yalifungwa na Clement Mzize, aliyetupia mawili, Prince Dube na Stephane Aziz Ki, kila mmoja akifunga goli moja.

Ramovic, tayari ameiongoza Yanga kushinda michezo minne ya Ligi Kuu, akianzia dhidi ya Namungo aliposhinda mabao 2-0, Mashujaa FC (mabao 3-2), Prisons na Dodoma Jiji kila timu ikipata kipigo cha mabao 4-0.

Hata hivyo, ushindi huo unaendelea kuwabakisha katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi baada ya kufikisha pointi 36, nyuma ya vinara Simba wenye pointi 37.

Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime, alisema timu yake ilistahili kufungwa.

"Tumestahili kuadhibiwa, ukiangalia mabao yote manne ni wachezaji kutojiamini, kufanya makosa yale yale ya kujirudia na kuwapa mipira wachezaji wa Yanga, wanatufunga, kwa hiyo tutakaa chini tuangalia nini turekebishe na kama kuna nguvu inatakiwa iongezwe, yaani kusajili wachezaji kipindi hiki cha dirisha dogo, basi tuongeze," alisema kocha huyo.

Yanga itarejea tena uwanjani keshokutwa kuwakaribisha Fountain Gate na baada ya hapo itaanza maandalizi ya kuikaribisha TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo) kwa ajili ya mechi ya raundi ya nne ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa Januari 3, mwakani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.