WACHEZAJI wa Namungo FC, wamekiri usajili wa wachezaji wapya katika dirisha dogo limeongeza nguvu ndani ya kikosi chao na kusaidia kutopoteza mechi katika michezo yao mitatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa hivi karibuni.
Namungo imeshinda mechi mbili za ugenini na kutoka sare mara moja nyumbani na sasa imefikisha pointi 17 na kupanda hadi nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Nahodha wa Namungo, Erasto Nyoni, alisema hayo baada ya kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani, Manyara ambapo timu yao ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Fountain Gate.
Nyoni, ambaye ni beki wa kati, amesema hata wachezaji wa zamani wamefurahia ujio wa nyota hao wapya kwa sababu wameongeza nguvu kikosini tofauti na walivyokuwa awali.
"Kusema kweli wachezaji wapya waliosajiliwa kipindi hiki cha dirisha dogo wamekuja kuongeza nguvu kubwa katika kikosi, kinaonekana kuimarika, tunawashukuru sana na sisi waliotukuta tunawapa sapoti kubwa ndiyo maana unaona kuna mafanikio," alisema Nyoni.
Nyota wapya waliosajiliwa na Namungo mpaka sasa ni kiungo, Najib Mussa kutoka Singida Black Stars na mabeki waliorejea, Derrick Mukombozi na Emmanuel Charles.
"Ilikuwa mechi ya kisasi, katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Fountain Gate walishinda kwetu na sisi tumekuja kuwafunga kwao, hiyo ni sehemu ya mchezo, nawashukuru wachezaji wangu kwa kazi kubwa walioifanya," Juma Mgunda, Kocha Mkuu wa Namungo, alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED