SIKUKUU ya Krismasi imemalizika sasa inafuata Mwaka Mpya wa 2025, ambayo kama Mwenyezi Mungu atatujalia kuwa hai, tutaisherehekea Jumatano ijayo. Ni kama siku tano zijazo.
Kwa wale ambao tumebahatika kuifikia Krismasi, hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ulinzi wake kwetu kila uchao, kwani wapo baadhi yetu ambao walitangulia mbele ya haki siku chache kabla ya sikukuu hiyo.
Tunapokaribia kufikia mwaka mpya, ninaomba nitumie nafasi hii kuwatakia sikukuu njema yenye baraka tele na amani, mle mnywe lakini kwa kiasi.
Lakini pamoja na hayo, ninapenda kuwakumbusha wenzetu wafanyabiashara, kuepuka kupandisha bei vitu na kusababisha watu kushindwa kumudu bei.
Mtindo huo ambao umekuwa ukijirudia kila wakati wa sikukuu, ni mwiba kwa watu wa kipato kidogo ambao hudunduliza pesa, ili angalau wakati wa sikukuu wale vizuri na wawe sehemu ya kicheko hicho .
Ingependeza kama wakati wa sikukuu, tukaona bidhaa nyingi katika maduka ingekuwa zinapunguzwa, ili kuwawezesha watu wote kumudu kununua mahitaji na kufurahia sikukuu hiyo.
Wakati wa Sikukuu ya Krismasi, tumeshuhudia wafanyabiashara wa nyama wakipandisha bei kutoka shilingi 10,000 kwa kilo hadi kufikia shilingi 12,000. Hiyo ni bei ya Dar es Salaam, lakini tumeambiwa katika vyombo vya habari nyendo ni hizo, kupanda bei kila kona, kulingana na wastani wake.
Hapo tuweke nukta kutafakari, jamani wa hali ya chini wataserebuka vipi?
Kwa mtindo huo ni kwamba wale ambao hula nyama mara moja kwa kulingana na kipato chao, hawawezi kumudu bei hiyo.
Ni vyema wakati kama huo, ndio ambao bei za bidhaa zingekuwa za kawaida kama njia mojawapo ya wafanyabiashara kuonesha kuwa wanawajali wateja wao wenye uwezo wa kipato na wa kawaida.
Ninadhani kipindi cha sikukuu kisingetumiwa na baadhi ya wafanyabiashara kujinufaisha zaidi, bali wawajali wateja wao bila kuangalia uwezo wa kipato au kujali maslahi makubwa tu.
Ikumbukwe kuwa msimu wa sikukuu ndio ambao kila mtu hujitutumua nyumbani kwake kinapikwa chakula kizuri, watoto wanatoka na nguo mpya, hivyo ingependeza kama hawataumizwa na bei ya bidhaa madukani.
Lakini mtindo wa kuvizia msimu wa sikukuu na kupandisha bei ya bidhaa, ni sawa na kukomoa watu sasa wafanyabiashara walione tatizo hilo na kulitafutia ufumbuzi haraka ili kuwapa unafuu wateja wao.
Inaumiza kuona, kitu ambacho ulinunua jana kwa shilingi 8,000, unakuta leo kinauzwa shilingi 10,000. Kwanini bei ipande ghafla kiasi hicho, kuna nini hapo katikati?
Ni kweli bidhaa itapanda na wateja watakuja tu, lakini kumbukeni kuna kundi lingine nyuma linakwama kupata mahitaji ya sikukuu kutokana na bei ya bidhaa kuwa juu.
Jambo la kuzingatia ni kwamba wale wote wanaofanya biashara iwe kubwa au ndogo, wasitumie mwanya huo kujinufaisha au kuufanya msimu wa sikukuu kama kipindi cha mavuno kwao.
Ninaamini kila mmoja awe na uwezo mkubwa au mdogo kifedha, anatamani angalau siku ya sikukuu ajitutumue anunue chochote atumie na familia yake.
Vilevile, huyo anayejitutumua na mwanzo wa mwaka, ndiye mhanga wa janga la gharama za lazima, ikianzia na kinara wao ada na gharama za shule kwa wanafunzi.
Hivyo, enyi wafanyabiashara na mamlaka zinazohusika pale inapobidi, tumieni uungwana kuhakikisha mnachangia kuzuia mfumuko wa bei wa ghafla ambao husababisha maumivu kwa baadhi ya watu hasa wa kipato cha chini.
Wafanyabiashara wakubwa, wadogo na wachuuzi wote tunaelekea katika sikukuu ya mwaka mpya, muangalie uwezekano wa kuhakikisha kila mteja anapata anachokitaka kulingana na uwezo wake kiuchumi.
Niwatakie maandalizi mema ya sikukuu ya Mwaka Mpya, uwe wa heri na fanaka, atakayejaliwa kufikia, atimize yote mema aliyokusudia kuyafanya kwa mwaka 2025.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED