KIPINDI cha msimu wa Krismasi na Mwaka Mpya, imekuwa kawaida ya vijana kuunda mikusanyiko isiyo na manufaa.
Staili zao huwa wanatengeneza magenge ya uhalifu, wakiamini kupitia mikusanyiko hiyo itazaa matunda kiuchumi kwao.
Dhana yao kuu, wanafikiri kwamba watu kwa nyakati hizo wanakuwa na ‘chochote kitu’ kwa sababu wamejikusanyia kipato kwa matumizi ya sikukuu hizo.
Hilo linatolewa ufafanuzi na kijana Salehe Hassan, mkazi wa Mbezi Matosa wilayani Ubungo, Dar-es Salaam, anayesema nyakati za sikukuu, kumekuwapo matukio ya uporaji wa simu na hasa kwa wanawake wanaotoka kuwatembelea ndugu zao.
Anatamka kwamba, vibaka na wahuni hutumia mazingira hayo kufanya uhalifu tajwa.
Kwa mujibu wa Salehe, cha msingi kinachotakiwa kuwapo ni ulinzi shirikishi nyakati za usiku na mahali penye ukabaji.
Kunatajwa suala la kukabwa, kukabana linatakiwa kushughulikiwa kwa nguvu za kisheria kabla ya hazijavuka mbali.
Hapo kijana huyo wa Mbezi ananena lake, akiwataka wahusika hao waache kufanya hivyo, maana ina wapelekea katika hatua zingine, wapo wanaochukua hatua za mkononi, falsafa zao zikiwaambia wako sahihi .
Vilevile, mkazi mwingine anayejitambulisha kwa jina, Joseph Pascal , ni kwamba nyakati za sikukuu wanakumbana na mikasa kama hiyo, akitaja maeneo mengine kama Mwananyamala, wilayani Kinondoni, kuna mambo ya aina hiyo.
Anasema, kuna watu wengine wanaojishughulisha na wizi, kama sehemu ya kutimiza wajibu wa kiuzazi katika familia yao na ili kupata chakula bora.
Msemaji huyo anataja watu hao inawalazimu waingie mtaani na kufanya ‘ukwapuzi’, jambo linaloweka maisha yao hatarini, kwani wanakuwa jirani na kifo ama kwa kipigo au kutiwa nguvuni kwenye vyombo vya serikali.
Hivyo ni muhimu watu kujipa majukumu sahihi na wanayoyaweza na wasiyoyaweza waachane nayo.
Jeshi la Polisi nchini, nalo linasema kuwa hali ya usalama wa nchini iko shwari, huku likibainisha kuwapo uhalifu mkubwa na mdogo unaoendelea kudhibitiwa kupitia mikakati mbalimbali iliyobuniwa.
Hiyo inatajwa kuendelea kutekelezwa kwa kushirikisha wananchi na wadau wengine wanaozuia uhalifu wa kijinai nchini.
Akitoa taarifa yake, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, SACP David Misime, anasema katika kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka, jeshi hilo linaorodhesha mikakati ya kuhakikisha wanaendelea kuelimisha na kuzuia uhalifu, kufanya misako na operesheni kuwakamata wavunja sheria.
SACP Misime anasema kuwa polisi inawatahadharisha wazazi na walezi katika sikukuu hizo za mwisho wa mwaka, kutokuwaruhusu watoto kwenda kwenye maeneo ya mikusanyiko bila uangalizi sahihi.
Polisi nchini inasema, hali ya usalama wa nchi ni shwari, huku likibainisha kuwa uhalifu mkubwa na mdogo unaendelea kudhibitiwa kupitia mikakati iliyobuniwa na kuendelea kutekelezwa kwa kushirikisha wananchi na wadau wengine katika kuzuia uhalifu wa kijinai hapa nchini.
Anashauri hali ya kuwapo busara kwa kila mtu kutambua nyakati za sikukuu ni za upendo na ushirikiano kwa kila mmoja.
Hivyo, anataja ni vyema watu kukubaliana na hali zao na siyo kujipa majukumu asiyoyaweza au yasiyopendeza akitoa mfano wa kumdhuru mwingine, kutaka kupata chochote, kwani huwa na mwisho mbaya.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED