Karia kuendelea urais TFF, sawa ila atuondolee madudu haya

By Mhariri Mtendaji , Nipashe
Published at 11:38 AM Dec 23 2024
Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu.
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu.

KUNA asilimia kubwa rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Wallace Karia, akachaguliwa tena kuendelea kuongoza kwa kipindi kingine, baada ya wajumbe wengi kuonekana kuridhishwa na utendaji wake.

Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu na rais wa Klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said, wao waliuomba Mkutano Mkuu uliofanyika Moshi, Kilimanjaro, Jumamosi, kumpitisha moja kwa moja kutokana na kuridhishwa na kazi kubwa aliyoifanya kwa miaka saba aliyokaa madarakani.

Hata hivyo, Makamu wa Kwanza wa rais, Athumani Nyamlani, alijibu kuwa njia bora ya kufanya hivyo ni wanachama wote wa shirikisho hilo kumwekea dhamana mara akishachukua fomu ya kuwania urais na si kumpitisha moja kwa moja kwa kutofanya uchaguzu kama viongozi wa Simba na Yanga walivyoshauri.

Kwa ujumla, tunathamini mchango wa viongozi wa klabu hizo kongwe, lakini tunapongeza uamuzi wa Nyamlani wa kusimamia demokrasia kuwa uchaguzi ni lazima ufanyike, kwani vyama vinavyosimamia demokrasi uchaguzi huwa ni suala la kikatiba.

Tukirudi upande wa Karia ni lazima apongezwe kwa kiasi kikubwa kurudisha heshima ya shirikisho hilo na kulifanya kuaminika na taasisi kubwa na kampuni mbalimbali nchini tofauti na miaka ya nyuma.

Hakuna asiyejua kuwa taasisi ya mpira wa miguu, hasa wakati huo ikiitwa Chama cha Mpira Miguu nchini (FAT), ilikuwa haiheshimiki, kukubalika na wala kuaminika.

Ni chama kilichokuwa kikikumbwa na migogoro ya mara kwa mara kwa viongozi wenyewe kwa wenyewe na hata kwa taasisi zingine. Pamoja na kwamba mpira wa miguu ulikuwa ukipendwa sana, lakini bado haukuwa kwenye mifumo sahihi na ya kisasa kama hivi leo.

Huko nyuma tuliona hata pesa za viingilio zikichukuliwa kwenye viroba na kupelekwa benki au kulala ofisini. Hata wachezaji walikuwa wakisajiliwa kwa kuwekewa lundo la noti mezani.

Leo hii imekuwa historia. Kila kitu kinafanyika kwenye mifumo sahihi ya kipesa, kama vile benki na mifumo mingine ya kiserikali.

TFF imekuwa ni Shirikisho linaloaminika na kampuni nyingi iwe ndani na nje ya nchi, hivyo kuzivutia kudhamini ligi na michuano mingine.

Kabla ya Karia kuingia madarakani, Tanzania ilikuwa imefuzu AFCON mara moja tu, lakini wakati wa utawala wake imefanya hivyo mara tatu kiasi kwamba kutinga hatua hiyo kwa sasa kwa Taifa Stars si habari kubwa tena.

Klabu kama Simba na Yanga zimefanya vizuri sana kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho na kwa sasa kuwa moja ya nchi inayoogopewa kwenye mashindano mbalimbali ya klabu barani Afrika, hapo huwezi kukwepa juhudi za Karia.

Ligi ya Tanzania kwa sasa ipo nafasi ya sita kwa ubora. Timu za Vijana nazo na za wanawake huwezi kuziacha kwa kufanya vema. Yote hii ni chini ya utawala wake.

Pamoja na yote bado haiwezekani apitishwe tu moja kwa moja bila uchaguzi. Tuna uhakika kuwa atachaguliwa kuendelea kuwa rais wa TFF kwa hiki kinachoonekana, lakini kwa sasa kuna vitu anavyotakiwa kuviondoa ili amalize kwa amani na kuwa kiongozi wa kukumbukwa.

Kwanza ni kuifanya ligi ya Tanzania kuwa na waamuzi bora, kuanza kutumika kwa VAR, pamoja na kuondoa kampuni moja kudhamini klabu zaidi ya moja.

Yatasemwa yote, lakini hili ni doa kwenye mpira wa Tanzania. Mdhamini aliyewekeza kwenye timu moja kudhamini tena timu zingine ni moja ya mambo ambayo wadau wengi wa soka wanalalamikia na ni lazima lipatiwe ufumbuzi kwa kuondolewa kitu kama hicho.

Haya ndiyo mambo ambayo Karia anapaswa kuyaondoa kuanzia msimu ujao ambao atakuwa akianza muhula mpya wa uongozi wake endapo akichaguliwa.