MGANGA wa kienyeji, Juma Lugendo (30), mkazi wa Kahama, mkoani Shinyanga, amekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida akidaiwa kusafirisha vifaa vya uganga na dawa za kienyeji zilizochanganywa na utumbo mbichi wa samaki ndani ya basi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Amon Kakwale, katika taarifa yake jana kwa vyombo vya habari, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Desemba 19 mwaka huu saa 12:30 jioni, maeneo ya mlima Sekenke, kata ya Ulemo wilayani Iramba, mkoani Singida.
Alisema mtu huyo alikuwa anasafirisha vitu hivyo ndani ya basi la kampuni ya Frester lenye namba za usajili T 794 EHR lililokuwa linatoka Kahama kwenda Dar es Salaam.
Kamanda Kakwale alisema polisi waliokuwa doria katika barabara ya Singida-Nzega, walipata taarifa zilizoenezwa kupitia mitandao ya kijamii kwamba ndani ya basi hilo mlikuwa na mtu aliyekuwa anasafirisha kichwa cha mtoto ambacho kilikuwa kinatoa harufu mbaya na kusababisha kero kwa abiria wengine.
Alisema kuwa baada ya kupata taarifa hizo, polisi waliweka mtego na kumkamata mtuhumiwa huyo na kumpeleka katika kituo kidogo cha polisi cha Misigiri ambako baada ya upekuzi, alikutwa na vifaa vinavyotumika katika uganga wa kienyeji na dawa za kienyeji ambazo zimechanganywa na utumbo mbichi wa samaki.
Kamanda Kakwale alisema mtuhumiwa baada ya kukamatwa, alifikishwa mahakamani akikabiliwa na kosa la kufanya shughuli za uganga wa kienyeji bila kuwa na kibali.
"Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa wananchi wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kutoa taarifa za uongo na kusababisha taharuki kwa jamii," ilieleza taarifa hiyo ya Kamanda Kakwale.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED