HIVI sasa kuna mradi wa ujenzi wa soko la kisasa la Tandale uliopo Dar es Salaam, ambao ni wa kimkakati, kukitarajiwa kuingizia Halmashauri ya Wilaya Kinondoni Sh. milioni 2.5 kila siku.
Hiyo ni sawa na Sh. milioni 75 kila mwezi, vivyo hivyo wastani wa shilingi milioni 912 kila mwaka.
Kimsingi, ujenzi wa soko hilo wenye thamani ya Sh. bilioni 10.2, ulianza mwaka 2013, kwa fedha kutoka serikali kuu, sasa wafanyabiashara waameanza kulitumia, huku taratibu za kulizindua rasmi ukiandaliwa.
Wafanyabiashara wa soko hilo lililojengwa kisasa likiwa na ghorofa mbili walianza kuingia ndani Oktoba mwaka jana na sasa wanaendelea na biashara zao kama kawaida.
"Soko lilikamilika na kuanza kazi rasmi, litakuwa linaiingizia Manispaa ya Kinondoni mapato ya Sh. milioni 2.5 kwa siku,” anatamka Mweka Hazina wa Manispaa Kinodoni,’ Onesmo Mwonga.
Anafafanua hayo, katika ziara ya Katibu Tawala wa mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Toba Nguvila, hivi karibuni alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wake.
Katika maelezo yake ni kwamba, soko hilo lina vitengo mbalimbali ambavyo manispaa itaweze kukusanya Sh. milioni 2.5 kila siku kutoka kwa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao humo.
Anafafanua kuwa, ujenzi wa soko hilo umefikia asilimia 99 na kwamba utaratibu wa kupanga wafanyabiashara umefanywa kwa kuzingatia mahitaji ya kila mfanyabiashara na aina ya bidhaa wanazouza.
Ofisa Biashara, Viwanda na Uwekezaji wa Manispaa Kinondoni, Phillipo Mwakibete, anasema matarajio ya manispaa ni kuona wafanyabiashara wote wakinufaika na fursa hiyo ya kuwa na soko la kisasa.
"Soko litawezesha wafanyabiashara kuuza bidhaa zao katika mazingira safi na salama, na kwamba soko la hilo lina zaidi ya wafanyabiashara 2000 wa vitendo mbalimbali wakiwamo mama lishe na baba lishe.
CHANGAMOTO
Mwenyekiti wa soko hilo, Sultan Kiumbo, anasema pamoja na hatua zilizochukuliwa na manispaa kuliboresha kuwa la kisasa, bado kuna changamoto inayowakabili.
Kiumbo anaitaja kuwa, ni ukosefu wa usafiri wa daladala za kufika sokoni hapo, hali inayosababisha wateja kwenda katika masoko mengine, ambayo yanafikika kirahisi.
"Soko letu liko maeneo ya katikati ya Tandale, hakuna daladala zinazofika hapa, bali zinashusha abiria kwa Mtogole Kwa Tumbo (Barabara kuu ya Magomeni- Sinza), au Manzese Argentina (Barabara Morogoro) ambako ni mbali halafu njiani kuna vibaka, hivyo wateja wanaohofia usalama wao," anasema Kiumbo.
Mwenyekiti huyo anafafanua kuwa, muda wa wateja kufuata bidhaa sokoni huwa ni alfajiri na kwamba muda huo ndio ambao pia ‘vibaka’ huwinda watu kuwapora mali zao.
"Katika mazingira hayo, ni vigumu mteja kushuka Kwa Mtogole, Kwa Tumbo au Argentina afajiri ili afuate bidhaa Tandale, badala yake anakwenda soko lingine kwa ajili ya usalama wake," anasema.
Kiumbo anasema anatamani soko hilo liwe kama masoko ya Temeke, Simu 2000, Mabibo na mengine ambayo yanafikika kirahisi wakati wote bila usumbufu wala hofu kwa wateja.
Anasema sio vibaya daladala zikawa zinashuka abiri na kuendelea na safari za kwenda katikati ya jiji, Ubungo, Mabibo, Makumbusho na maeneo mengine ili iwe rahisi kwa wateja kufika sokoni hapo.
"Soko letu lina vitengo vingi vikiwamo vya mazao ya nafasi, mama lishe na baba lishe, viazi vitamu, viazi mviringo, nafaka, mihogo, miwa na vingine vingi vinavyoweza kuingizia manispaa mapato ya kutosha, kwani ushuru ukiwaamo unaoanzia shilingi 500 kwa siku," anasema.
MAAGIZO YA RAS
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Toba Nguvila, anamuagiza Katibu Tawala wa Manispaa ya Kinondoni na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, kukutana na viongozi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kupanga ‘ruti’ za kufika sokoni hapo.
Dk. Nguvila anatamka kuwa, changamoto mbalimbali zilizopo sokoni hapo zitatuliwe haraka ikiwamo pia kuboresha mfumo na vyoo ili kuondoa malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara.
Anafafanua kuwa lengo ni kuhakikisha wafanyabiashara wanaendesha shughuli zao bila usumbufu, huku wateja wao nao wakija kupata huduma bila kikwazo chochote hasa kwa upande wa usafiri.
Kiongozi huyo anaongeza kuwa kuna haja ya soko kuwa ua jenereta kubwa ambalo litasaidia biashara kufanyika muda wote bila usumbufu wa ukosefu wa umeme, kwa kuwa ni soko la kisasa.
"Wito wangu ni kwamba kusiwe na kero au changamoto zozote zikiwamo za mafuriko wakati wa mvua, badala yake kazi ifanyike kuhakikisha soko linafanya kazi kwa ufanisi.," anasema Dk. Nguvila.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED