BANGROS Sikaluzwe (37), mkazi wa Ilolo, wilayani Mbozi, amekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kwa tuhuma za kujifanya askari wa Jeshi la Polisi nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Akama Shaaban, mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 22 mwaka huu saa 7:45 usiku katika msako uliofanyika Mtaa wa Majengo, mjini Tunduma, katika wilaya ya Momba.
Kaimu Kamanda Akama alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa anafanya kazi za usalama barabarani katika barabara ya Tunduma-Sumbawanga kwa kuyapanga malori yanayovuka mpaka wa Tunduma kwenda Zambia na nchi nyingine za kusini mwa Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Kaimu Kamanda Akama, mtuhumiwa huyo alikutwa akiwa amevaa sare za polisi. Pia anadaiwa kukutwa na vifaa vingine vya jeshi hilo, zikiwamo pingu alizokuwa amezining’iniza kiunoni, kisu cha kukunja na tochi aliyokuwa ameshika mkononi.
Kaimu Kamanda Akama alisema kuwa uchunguzi wa haraka ulibaini kuwa Sikaluzwe siyo askari polisi, bali ni mgambo aliyekuwa anajifanya askari kwa malengo ambayo hayajathibitishwa.
"Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limewaonya wananchi, waache tabia ya kuvaa sare za polisi au kujifanya askari, kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika," Kaimu Kamanda Akama anaonya katika taarifa yake hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED