Serikali kuingia mkataba ujenzi SGR Uvinza-Bujumbura, hadi Kindu DRC

By Hamida Kamchalla , Nipashe
Published at 04:02 PM Jan 24 2025
 Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa alipotembelea  kipande cha sita cha ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka mkoani Tabora hadi Kigoma.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa alipotembelea kipande cha sita cha ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka mkoani Tabora hadi Kigoma.

SERIKALI inatarajia kuingia mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Uvinza mkoani Kigoma hadi Bujumbura nchini Burundi ambapo baadaye kuendelezwa kutoka Bujumbura hadi Kindu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

 Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameyasema hayo jana alipotembelea kipande cha sita cha ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka mkoani Tabora hadi Kigoma yenye urefu wa kilometa 506, mradi unaogharimu kiasi cha sh. trilioni 6.3 huku mradi huo ukitarajiwa kukamilika Machi 2027. 

“Wale wanaosema Kigoma ni mwisho wa reli, miaka miwili au mitatu ijayo hilo jambo litabadilika na Kigoma sasa itakuwa ni katikati ya reli,” amesema Mbarawa. Alisema kwa muda mrefu kumekuwa na kero mbalimbali ambazo mkandarasi amezieleza lakini waatalamu wapo na wanazifanyia kazi, ambazo nyingi ni za kihandisi na kuwahakikishia wananchi kuwa kazi hiyo itakwenda kwa kasi inayotakiwa. 

Meneja wa mradi huo Mhandisi Wallace Isaya amesema kuwa ujenzi huo umekuwa na kero katika eneo la mto Maragarasi kutokana na mvua nyingi ambazo huleta athari kwa kipindi cha takribani miezi saba kila mwaka. "Lakini pia pamoja na kuwepo na kero hiyo, katika msimu wa kiangazi uliopita, mkandarasi amefanikiwa kujenga nguzo 13 za daraja hili, amebainisha Mhandisi Isaya.