NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu, Patrobas Katambi amesema mfumo wa kielektroniki wa Taarifa na Kanzidata ya Watu wenye Ulemavu (PD-MIS) utasaidia Serikali kupanga mipango ya huduma wezeshi kwa watu Wenye Ulemavu nchini.
Amesema hayo Jijini Mwanza wakati akifungua mafunzo ya mfumo huo kwa maafisa ustawi wa jamii na TEHAMA wa Halmashauri na mikoa ya Mwanza, Kagera, Geita, Simiyu, Shinyanga na Mara amesema Serikali imedhamilia kuhudumia kundi la Watu Wenye Ulemavu.
Aidha,Katambi amesema lengo la mfumo huo ni kukusanya taarifa na takwimu za watu wenye Ulemavu kuanzia kwenye mtaa na vijiji ili kusaidia kupata taarifa sahihi na kuongeza ufanisi na upatikanaji wa huduma kwa kundi hilo maalum.
Vile vile, amebainisha kuwa mfumo huo utasaidia watoto wanaozaliwa na ulemavu kutambulika mapema na kupatiwa huduma za marekebisho ili kubadilisha maisha yao.
"Kukosa taarifa sahihi kunawafanya watu kuwa na ulemavu wa kudumu ambao kama ungegundulika mapema ungerekebishwa, hivyo mfumo huu utasaidia sana Serikali kuwatambua, kuwasikiliza changamoto zao na kuwahudumi," amesema Katambi.
Naye Mkurugenzi Msaidizi huduma za ustawi wa jamii Ofisi ya Rais TAMISEMI, Subisya Kabuje amesema mfumo huo utasaidia kupata taarifa sahihi za makundi yote ya watu wenye ulemavu na kuisaidia wizara kupanga mipango na huduma kwa makundi hayo.
Awali akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo huo Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Dkt. Edith Rwiza amesema ofisi hiyo itahakikisha ina simamia mfumo huo ili kuleta matokeo yenye tija yaliyokusudiwa na serikali kwa walengwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED