Katambi atamba kutekeleza ilani ya CCM kwa asilimia 100

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 08:12 PM Jan 24 2025
Mbunge wa jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi akisoma taarifa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi CCM 2020 hadi 2024
Picha:Marco Maduhu
Mbunge wa jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi akisoma taarifa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi CCM 2020 hadi 2024

Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, amesoma taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020/2024, akisema ameitekeleza kwa asilimia 100.

Taarifa hiyo aliwasilisha leo Januari 24, 2025, mbele ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Shinyanga Mjini, ambapo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Ally Hapi, alikuwa mgeni rasmi.

Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), amebainisha mafanikio katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu, afya, miundombinu, maji, na nishati safi ya kupikia.

Mafanikio Makuu

Elimu

Mbunge Katambi amesema ndani ya miaka minne, shule mpya tisa zimejengwa, zikiwemo shule za msingi tano na sekondari nne. Aidha, alifanikiwa kuanzisha tawi la Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo na kupanua Chuo Kikuu cha Moshi (KICoB) tawi la Kizumbi.

Miundombinu

Katambi ameeleza kuwa miundombinu ya barabara, madaraja, na masoko imeboreshwa. Alitaja ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Ibadakuli, daraja la Uzogole, na maboresho ya barabara katika maeneo ya Iwelyangula, Ibinzamata, Ndala, Ihapa, Mwamalili, na Mwanoni.

1

Afya

Ameboresha huduma za afya kwa kujenga vituo vya afya, zahanati sita, na hospitali, ikiwemo Kituo cha Afya Kambarage na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. Pia, alitoa ambulensi sita kwa msaada wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Maji

Amesema mtandao wa maji umeongezwa katika maeneo ya Bugwandege, Masekelo, Mwamasheke, Mwanubi, Busongo, na maeneo ya mjini. Zaidi ya shilingi bilioni 195 zimetengwa kwa usambazaji wa maji kwa kipindi cha 2024/2025.

Mikopo na Ajira

Ameeleza kuwa shilingi milioni 200 zilitolewa kwa vikundi vya Boda boda, Bajaji, wanawake, na watu wenye ulemavu kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga. Pia, milioni 19 zilipatikana kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu.

Nishati Safi

Katambi amegawa mitungi ya gesi 1,780 kwa makundi mbalimbali ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

2

Michezo

Mbunge huyo alianzisha ligi mbalimbali za michezo, ikiwemo utoaji wa zawadi za hadi shilingi milioni 6 kwa washindi wa mashindano.

Wito kwa Wana-CCM

Katambi amewataka wana-CCM kushirikiana kwa ajili ya maendeleo na kuepuka migogoro. Aliwasihi viongozi wa chama kuendelea kushirikiana kwa manufaa ya wananchi.

Pongezi na Tahadhari za Viongozi wa CCM

Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Odilia Batimayo, amempongeza Katambi kwa kazi nzuri na alionya dhidi ya kampeni za mapema za kugombea ubunge. Ally Hapi naye alimsifu Katambi kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM, akisema mafanikio hayo yanaongeza imani ya wananchi kwa chama.

Hapi amewataka wagombea kuzingatia maadili ya chama, kujiepusha na wapambe wa kisiasa, na kuendeleza siasa za kisayansi kwa kujenga hoja kwa wananchi.

Katika hafla hiyo, Katambi pia amekabidhi kiti mwendo kwa mtoto mwenye ulemavu, Delfina Mashaka, na vifaa vya sauti kwa uongozi wa Stendi ya Mabasi ya Mkoa wa Shinyanga.