FELISTER Hassan, mama mzazi wa Mwenyekiti mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu amesema amefurahishwa na ushindi wa mwanawe aliopata juzi, akitarajia kuona mabadiliko makubwa yakitokea ndani ya chama hicho.
Akizungumza juzi na waandishi wa habari katika kijiji cha Mahambe wilayani Ikungi, mkoani Singida, mama huyo alisema ushindi huo umemfurahisha na anamwombea mwanawe majukumu mema ya kujenga chama.
"Baada ya kusikia mwanangu ameshinda, nilijisikia vizuri, nikapiga na vigelegele, nilifurahi sana, nikasema 'Mungu ni mwema'. Nilikuwa ninamwombea sana ashinde, nikasema 'mwanangu aingie na amjalie aendelee vizuri na kazi aliyoipata, aishi vizuri'," alisema.
Mama huyo pia alitaja sababu za mwanawe huyo kupewa jina la "Tundu", akibainisha kuwa ni la ukoo la kabila la Kinyaturu ambalo alipewa na baba yake.
Dada wa Lissu, Alu Lissu, alisema kuwa yeye pamoja na ndugu zake 10 tangu asubuhi ya Jumanne hadi saa 7:00 usiku wa kuamkia Jumatano, walikuwa wanafuatilia uchaguzi huo wa CHADEMA na kwamba juzi saa 12 asubuhi waliamka mapema kupata matokeo.
"Ni kama hatukulala tu, tulikesha tukiomba na kufuatilia uchaguzi huu. Tunamshukru Mungu maombi yetu yamekubalika hadi ndugu yetu ameshinda.
"Kwa furaha tuliyonayo hapa nyumbani ni lazima leo (juzi) tuchinje kuku na ikiwezekana hata ng'ombe," alisema Alu.
Dada huyo wa Lissu alisema ushindi wa kaka yake unakwenda kuleta mabadiliko ndani ya CHADEMA kutokana na Lissu kuwa jasiri, mpenda haki na anayetaka mabadiliko katika kazi anayofanya.
Majirani wa nyumbani kwa kina Lissu, Consolata Zacharia na Marcel Bilal, walisema CHADEMA sasa imepata jembe na mtu jasiri ambaye atakwenda kuinua chama hicho, wakidai kilikuwa kimeanza kupoteza mvuto kwa wananchi.
Katika uchaguzi huo, Lissu alipata kura 513 sawa na asilimia 51.5, akimwangusha Freeman Mbowe aliyekuwa anatetea kiti chake na Odero Charles waliopata kura 482 na moja, mtawalia.
Mbowe amekiongoza chama hicho kwa miaka 21 tangu alipochukua kiti cha uenyekiti mwaka 2003, akiwa ni mwenyekiti wa tatu tangu kuanzishwa kwa chama hicho, akitanguliwa na Edwin Mtei na Bob Makani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED