Vivuko vinne kukamilika mwezi Machi

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 07:35 PM Jan 24 2025
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega.

WAZIRI wa Ujenzi Abdallah Ulega amesema vivuko vinne kati ya sita vinavyotekelezwa nchini, chini ya Mkandarasi Mzawa Songoro Marine Transport Ltd vinatarajiwa kukamilika mapema mwezi wa tatu na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Ulega ametoa kauli hiyo leo Januari 24, 2025 jijini Mwanza wakati akikagua ujenzi wa vivuko hivyo vipya vitano kati ya sita vinavyokelezwa kwaajili ya kufanya safari katika maeneo mbalimbali ndani ya Ziwa Victoria.

Amesema serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa vivuko vipya sita pamoja na ukarabati wa vivuko vitatu ndani ya Ziwa Victoria, Bahari ya Hindi, Ziwa Tanganyika na Nyasa kwa zaidi ya Sh.bilioni 56.

Kadhalika amesema kati ya vivuko hivyo vivuko vipya vitano vinavyotekelezwa katika Ziwa Victoria vinagharimu zaidi ya Sh.bilioni 50 na kati ya hivyo vinne vinatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi wa nne.

Amesema kivuko kimoja kinajengwa jijini Dar es Salaam huku vinavyofanyiwa marekebisho ni pamoja na MV.magogoni, MV.Kigamboni na  MV.Nyerere.

1

“Nimpongeze Mkandarasi huyu mzawa kwa kuendelea kufanya kazi nzuri na kuaminiwa na serikali kutekeleza miradi mikubwa na kufanikisha kwa umaminifu mkubwa,”amesema Ulega. 

Awali Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd, wanatekeleza ujenzi na ukarabati wa vivuko hivyo,  Meja Songoro alisema utekelezaji wa vivuko hivyo utakamilika mapema hivi karibuni.

“Kivuko cha Bwiro-Bukondo chenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 100 kimefikia asilimia 91.3 kitakamilika Machi, 31 mwaka huu,  Nyegezi-Busorya asilimia 84.5 kinakamilika Marchi 29, Nyakariro-Kome 83.19 kinakamilika Machi, 29, Buyagu-Mbarika 88 kinakamilika Julai 4,” amesema Songoro.

Aidha amesema hadi vivuko vitano vya Ziwa Victoria kukamilika kampuni hiyo itakuwa inaidai serikali Sh.bilioni 12.417.