TRA kutumia mfumo mpya kuongeza mapato ya forodha

By Moshi Lusonzo , Nipashe
Published at 03:36 PM Jan 24 2025
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusufu Mwenda.
Picha: Mtandao
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusufu Mwenda.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua mfumo mpya unaotumia teknolojia ya akili mnemba kwa ajili masuala ya kodi ya biashara na forodha.

Akizunguma katika hafla ya uzinduzi wa tovuti na mfumo huo wa ulipaji kodi uliofanyika Dar es Salaam jana, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusufu Mwenda, Juma Mwenda, alisema mfumo huo unaoitwa TANCIS unaunganisha na taasisi 36 za serikali ikiwamo bandari, viwanja vya ndege na vituo vya forodha.

Alisema mfumo huo wa kisasa zaidi ambao umeanza kufanya kazi jana umetengenezwa na kampuni kutoka Korea Kusini utaleta mapinduzi katika ukusanyaji wa kodi nchini.

Mwenda alisema kwa kutumia mfumo huo wafanyabiashara hawatatakiwa kwenda ofisi za TRA kwa ajili a kulipa au kupata ufafanuzi wa kikodi, badala yake watafanya kila kitu wakiwa katika maeneo yao ya kazi.

 “Mfum huu unamuwezesha mfanyabiashara kuingiza bidhaa nchini, kujua gharama halisi ya kodi ya mizigo wake na kulipia kabla haujaingia bandarini, vianja vya ndege au katika vituo vya forodha vya mipakani. Njia hii italeta ufanisi katika biashara na kuondoa malalamiko ya wafanyabiashara, alisema Mwenda.

Alisema kutokana na taasisi zote zinazojihusisha na masuala ya kodi wanatumia, shughuli za kibiashara zitakuwa kwa kasi na kuondokana na tatizo la ucheleweshaji wa utoaji wa mizigo.

 “Kama wafanyabiashara wataingiza na kutoa bidhaa zao haraka bandarini, biashara zitaendelea kukua kwa kasi na mapato ya nchi yanaongezeka maradufu na kuinufaisha nchi kiuchumi,” aliongeza Kamishnahuyo mkuu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato, Uledi Mussa, alisema kukamilika kwa mradi huo ni kutekelezaji wa  agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alitaka kuwepo kwa mfumo ambao utasomana na taasisi zote za serikali.

“Nafurahi kuona kwamba agizo la Rais Samia tumelitekeleza na sasa taasisi zote zinazohusiana na masuala ya kodi watatumia mfumo huu wa TRA na kuwafanya wananchi kutumia muda mchache kukamilisha malipo au kupata huduma ya kikodi,” alisema Mussa.