Vivuko vyaongezwa kukabili kilio cha wakazi Kigamboni

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 11:26 AM Jan 24 2025
Vivuko vyaongezwa kukabili kilio cha wakazi Kigamboni.
Picha:Mpigapicha Wetu
Vivuko vyaongezwa kukabili kilio cha wakazi Kigamboni.

SHIDA ya usafiri kwa wakazi wa Kigamboni, Dar es Salaam imetatuliwa baada ya jana serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), ikishirikiana na sekta binafsi, kuzindua huduma ya vivuko viwili katika eneo la Magogoni-Kivukoni.

Mkataba wa ushirikiano huo umeingiwa kati ya TEMESA na Kampuni ya Azam Marine Ltd, ukigharimu Sh. bilioni 5.98 na utadumu kwa miaka minane kuwezesha usafirishaji abiria zaidi ya 50,000 kwa siku.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa vivuko hivyo, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega alisema kuwapo vivuko hivyo vya sekta binafsi, hakutaondoa vivuko vya serikali, bali abiria atakuwa na nafasi ya kuchagua.

"Kivuko kisiwe kikwazo cha watu kufanya biashara zao, au wanaokwenda hospitalini na kutoa huduma mbalimbali wakashindwa kufanya hivyo kwa wakati eti sababu tu kivuko kipo upande mwingine," alisema.

Waziri Ulega alisema vivuko vilivyopo vinapaswa kukaguliwa kila wakati na ndiyo maana vikifikia muda wa matengenezo, vinakwenda kukarabatiwa.

"Niwahakikishie kwamba vivuko vile vitakapokuwa tayari vitarejea hapa (Mv Magogoni na Mv Kigamboni) vitafanya kazi kwa ushindani na hiyo itatufanya tusibweteke na tuwe wabunifu na itafanya tuwe wabunifu," alisema.

Alisema kivuko cha Azam Marine kitavusha abiria, kikitumia dakika tano hadi sita kutoka upande mmoja hadi upande wa pili.

Alisema kiu ya serikali ni kuhakikisha watu wanaovushwa katika eneo hilo wanafikia 70,000 kutoka 60,000 wa sasa.

Waziri Ulega alishauri uongozi wa Azam Marine Ltd kuangalia uwezekano wa kwenda kuwekeza katika huduma za vivuko katika maziwa yote nchini.

Pia aliwaomba wavuvi katika eneo la Magogoni-Kigamboni kufanya shughuli zao bila kuathiri uvushaji wananchi.

Vilevile, alizitaka mamlaka zinazofanya ukaguzi, ziwe zinakagua mara kwa mara ili kuweka mazingira safi na ulinzi dhidi ya vitu vinavyoharibu vivuko, zikiwamo nyavu za wavuvi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Suleiman Kakoso, aliitaka serikali kutoa nafasi kwa wataalam wa ndani katika matengenezo ya vivuko.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema uwekezaji huo utatatua kero ya abiria kuchelewa kwenda kwenye shughuli za kijamii.

Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala alisema mkataba huo wa miaka minane unahusisha pia ujenzi wa majengo ya kupokea na kupumzikia abiria na ofisi.

Alisema mkataba huo pia utahusisha usimikaji mageti na mfumo wa ukusanyaji nauli na vivuko vya kasi vitatu. Mkataba ni wa miaka minane, lakini una makubaliano ya kufanyiwa mapitio kila baada ya miaka mitatu.

Kwa mujibu wa Kilahala, katika vivuko hivyo vya Azam Marine Ltd, abiria atatozwa Sh. 500 kwa safari moja.

Ujio wa vivuko hivyo, Kilahala alisema kutapunguza muda wa wastani wa dakika 45 ambazo abiria alikuwa anasubiri huduma. Sasa muda wa kusubiri huduma utakuwa chini ya dakika tano.

"Kwa sasa wakazi wa Kigamboni watakuwa na uhuru wa kuchagua kivuko ambacho wangependa kupanda kuvuka," alisema.

Aliongeza kuwa TEMESA inaendelea na utekelezaji ukarabati wa vivuko vya MV Kigamboni (umefikia asilimia 10) na Mv Magogoni (umefikia asilimia 55).

Matengenezo hayo kwa ujumla, Kilahala alisema yanagharimu Sh. bilioni 23.04.

Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Marine Ltd, Aboubakar Aziz alisema kati ya vivuko hivyo viwili, kila kimoja kitabeba abiria 250 kwa wakati mmoja.

Alisema vivuko hivyo vitaanza kutoa huduma saa 11:00 alfajiri hadi saa 5:00 usiku na vinakadiriwa kwa saa vitahudumia abiria 5,000 kwa siku.

Sambamba na vivuko hivyo viwili, Aziz alisema vingine vinne vinaendelea kujengwa na kabla ya Mei mwaka huu vitaanza kutoa huduma.

Kwa mujibu wa Aziz, kila kivuko kina injini mbili na vimekidhi viwango vya usalama vya Shirika la Uwakala wa Meli (TASAC).

Katika uwekezaji huo, Aziz alisema wamejenga majengo mapya ya kupokea na kusubiri abiria watakayotumiwa na vivuko hivyo.

Alisema Azam Marine Ltd kwa ujumla imetoa ajira za moja kwa moja 470 na inahudumia abiria milioni mbili kwa mwaka Tanzania Bara na Zanzibar.