Kombe la Chalenji kufanyika Juni

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 09:20 AM Jan 24 2025
Ofisa Mtendaji Mkuu wa CECAFA, Auka Gecheo
Picha: Mtandao
Ofisa Mtendaji Mkuu wa CECAFA, Auka Gecheo

MASHINDANO ya Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), yamepangwa kufanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, mwaka imefahamika.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa CECAFA, Auka Gecheo, aliliambia gazeti hili, kalenda ya mashindano yote ya ukanda huo yalipitishwa katika mkutano mkuu wa baraza hilo uliofanyika mjini Juba nchini, Sudan Kusini jana.

Gecheo alisema mkutano huo pia ulipitisha mashindano ya Kombe la Kagame (Dar Port Kagame Cup 2025), yatafanyika kuanzia Agosti 31 hadi Septemba 14, mwaka huu huku michuano ya soka la ufukweni itachezwa kati ya Mei 31 na Juni 7 nchini Kenya.

Alisema mashindano ya Chalenji kwa wanawake yatatangazwa baadaye huku michuano ya ngazi ya klabu ikipangwa kucheza kati ya Septemba 20 na Oktoba 4, mwaka huu.

"Vyama wanachama wa CECAFA wanatakiwa kutuma maombi ya kuwa wenyeji wa moja ya michuano hii iliyotangazwa ili kuhakikisha kalenda yetu ya mwaka 2025 itatekelezwa vyema," alisema Gecheo.

Red Arrows ya Zambia ndio mabingwa watetezi wa michuano ya Kombe la Kagame iliyofanyika Dar es Salaam mwaka jana wakati kwa wanawake, Simba Queens ya Tanzania Bara ilitwaa ubingwa wa michuano hiyo.