Tunaendekeza sana lugha, utamaduni wa kigeni!

By Joseph kulangwa , Nipashe
Published at 09:32 AM Jan 24 2025
Katuni
Picha: Muhidin Msamba
Katuni

KATIKA historia, kuna marehemu wawili huwakumbuka sana kutokana na misimamo yao ya kujitambua na hasa kutambua asili yao; mmoja Mwafrika na mwingine ni Mmarekani mwenye asili ya Afrika.

Mwafrika, kiongozi wa nchi aliyejulikana kama Mobutu na Mmarekani ni mwanamichezo mwanamasumbwi aliyeibuka kinara duniani na si mwingine, bali ni Muhammad.

Huyu Mobutu alizaliwa akiitwa jina la Joseph Desire na wazazi wake, baba yake akiitwa Mobutu. Lakini, baadaye akaona isiwe taabu, alipopata uraisi wa nchi iliyokuwa ikiitwa Congo, akabadili jina lake na la nchi.

Yeye akajiita Mobutu Sese Seko Kuku Ng’bendu wa Zabanga, huku nchi yake akiibadili jina na kuiita Zaire, akikataa kuitwa majina yaliyotoka kwa wageni waliokuja kututawala kwa maslahi yao binafsi, hivyo kutaka kutuvika utamaduni wao na wakafanikiwa.

Marekani akawapo manamsumbwi aliyejulikana kwa jina la Cassius Clay, jina la Wazungu hilo, akabadili na kusilimu akachukua jina la Muhammad Ali, ingawa si la kiafrika kwa asili, lakini angalau alikataa kasumba ya kigeni na kuendana na hili linalokubalika hata kwa Waafrika.

Wazaire walimwunga mkono Mobutu kwa kasi ya ajabu na karibu kila mmoja akakataa jina la kigeni na kubaki na la kikongo, hadi alipoingia madarakani Laurent Desire Kabila na ghafla Zaire ikawa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Waendelee kupumzika pema Mobutu na Muhammad!

Athari hasi hizi zimetamalaki katika mataifa mengi ya Kiafrika hasa yaliyotawaliwa na wageni hao, ambako majina ya Waafrika si ya kijadi tena, bali ya wageni, ingawa kuna baadhi ya makabila katika mataifa hayo, yameendelea kusimama kwenye majina yao ya asili.

Nchini mathalan, Wahadzabe wanastahili kuvuliwa kofia kwa kushikilia utamaduni wao, ingawa kuna wengine wanatakiwa kuelimishwa waachane nayo, ikiwa ni pamoja na ulaji nyama mbichi, pia kuchukulia kuoga ni kama anasa kwao. Yawezekana ni utamaduni, lakini uko hasi!

Nchini, tuko mstari wa mbele sana kujitapa na kujimwambafai, kuwa tunapigania na kudumisha utamaduni wetu, lakini kuna baadhi yetu imebaki kuwa nadharia isiyo kwenye vitendo, kwani tunashuhudia jinsi baadhi wanavyojisika anapolinganishwa au kufananishwa na kuwa wa jamii za mataifa hayo makubwa yaliyopiga hatua.

Chukulia mbongo utakayeonana naye mchana akiwa njiani kwenda baa, utazungumza naye Kiswahili kizuri mkaelewana, lakini akishakalia kigoda akaanza chupa ya kwanza, ya pili na kukaribia ya 10, Kiswahili kwishney, 

hajui tena, sasa anazungumza Kiingereza hata kama kibovu.

Tunashuhudia baadhi ya watangazaji wetu kwenye vyombo vyetu vya habari wakijadili mambo, hatawakosa kuchanganya na Kiingereza, ili mradi kujitanabahisha kuelewa somo vizuri, ingawa pia Kiingereza hicho ni tiamajitiamaji.

Huku kwenye majina ndiko usiseme, mtu anazaliwa na jina lake zuri tu na kusajiliwa kwenye cheti cha kuzaliwa, akipata elimu kidogo na pengine akaibuka nyota katika jambo fulani, hilo jina alilopewa na wazazi atalisigina na kuibuka na lingine angalau la Kizungu.

Wapo wanaojiita majina ya madini, ili mradi kuonekana wanang’ara na mbaya zaidi hata kujitambulisha rasmi wakitumia majina yasiyo rasmi kwenye vyeti vyao vya kuzaliwa au vitambulisho vya Nida! Huku kote ni kukanyaga asili na utamaduni! Kwani ukijiita jina la gari inakusaidia nini?

Tupo tunaojitapa sana kuenzi utamaduni na hasa lugha yetu, lakini hebu tazama vituo vingi vya habari hasa vya kielektroniki, vinavyotangaza kwa Kiswahili, vina mambo mengi ya kigeni wanavyorusha!

Hivi karibuni, sekta ya habari imepata Waziri mpya pia ni mwanahabari, Profesa Palamagamba Kabudi, ambaye anajinasibisha na kuhakikisha lugha fasaha ya Kiswahili inatumika katika kuwasilisha ujumbe na elimu kwa umma.

Namhurumia sana Profesa, kwamba anajitahidi sana, ila mafanikio ya hilo analotaka nahisi yako mbali, kwa sababu hivi sasa vyombo vyake vya habari vimejaa wasanii wasio na elimu ya lugha, bali kutangaza lolote linalowajia.

Tunahitaji mapinduzi makubwa katika kuhakikisha tunaendeleza Kiswahili fasaha, hasa kwa kuzingatia kuwa sisi ndilo chimbuko la lugha hiyo, lakini kuna kasoro za waendehaji vipindi.

Kwa namna hiyo, tuendako safari itakuwa ndefu sana, gari kuzimikia njiani. Tuna kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa, titi hili la mama ambalo ni tamu, linaendelea kutupa maziwa kwani hatuna kwingine kwa kunyonya, bali hapa hapa nyumbani. 

Tumwunge mkono Profesa Kabudi, huenda akatuvusha kutoka tope hili la uchafuzi wa lugha na utamaduni. Nilikuwapo!