WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana,amemvisha cheo na kumuapisha Dk. Elirehema Doriye, kuwa Kamishna wa Eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Balozi Dk. Pindi Chana, alimwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika hafla hiyo iliyofanyika Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha.
Waziri huyo amempongeza Dk. Doriye kwa kusimamia ongezeko la mapato, ambapo katika kipindi cha mwezi Julai hadi Novemba mwaka huu zaidi ya Sh. bilioni 138,680,341,953.65 zimekusanywa.
Huku, watalii 551,512 (watalii wa nje 350,091 na watalii wa ndani 201,421), wakitembelea eneo la hifadhi ya Ngorongoro katika kipindi cha miezi mitano.
“Nakupongeza kwa juhudi hizi kubwa ulizozifanya katika kipindi cha miezi minne iliyopita, endelea kuongeza juhudi katika usimamizi wa mapato, kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kuimarisha Mahusiano ya kikazi, Usimamizi wa haki za watumishi, mahusiano na wadau na kuongeza hamasa ya Utalii wa ndani ” aliongeza Balozi Chana.
Mwenyekiti wa Bodi ya wakurunezi wa NCAA, Jenerali Venance Mabeyo (Mstaafu) amempongeza Dk. Doriye kwa kuteuliwa, kuvishwa cheo, kuapishwa na kumuomba kuendelea kusimamia kikamilifu shughuli za uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii kwa kuzingatia misingi ya weledi, uzalendo, uvumilivu na kumsisitiza kuishi katika kiapo alichoapa katika kuanza majukumu mapya.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dk. Hassan Abbasi, amempongeza Dk. Doriye kwa uteuzi, kuhudhuria mafunzo ya jeshi la Uhifadhi na kuhitimu hivi karibuni na kumuwezesha kuvalishwa cheo na kuapishwa na kuwataka watumishi wa NCAA kutoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED