CHAMA cha Majaji Wanawake Tanzania(TAWJA) kimesema kuwa kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la kesi za ubakaji na ulawiti nchini.
Mwenyekiti wa TAWJA, Jaji wa Mahakama ya Rufani Barke Sehel alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya miaka 25 ya kuanzishwa chama hicho yatakayofanyika Januari mwakani jijini Arusha, mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
"Miaka ya nyuma kesi hizi zilikuwa chache na zilikuwa zinasikika katika baadhi ya mikoa tu, lakini miaka ya hivi karibuni mikoa yote ina matukio haya na yanafanyika kwa kiwango kikubwa. Hivyo, katika maadhimisho yetu, haya ni miongoni mwa mambo ambayo tutayazungumza.
"TAWJA tunafanya jitihada kuhakikisha changamoto hizi zinatatuliwa katika nyanja mbalimbali hasa kwa kutoa elimu katika eneo la usawa wa kijinsia na mambo mengine yanayofanana na hayo," alisema.
Jaji huyo alisema suala la mirathi kwa wanawake nalo ni eneo lenye kesi nyingi hivi sasa na wanawake ndio waathirika wakubwa wanaonyimwa kurithi mali hususani wanapofiwa na wenza wao.
"Kwahiyo tunaendelea kutoa elimu kwenye jamii kwa kuijengea uwezo kutambua haki zao hasa katika mirathi, talaka, haki za usawa na masuala mengineyo," alisema Barke.
Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho hayo, Sophia Wambura, alisema katika kipindi hicho cha miaka 25, TAWJA imefanikiwa kukuza hali ya usawa kwenye ngazi ya utendaji wa mahakama.
Jaji Sophia alisema tofauti na miaka ya nyuma, hivi sasa idadi ya wanawake majaji imezidi kuongezeka na kuwaongezea ari wanawake na wasichana wengi kuingia katika sekta hiyo licha ya kwamba hawajafikia kwenye ngazi ya juu ya uongozi katika eneo hilo.
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Aisha Bade alisema miongoni mwa mambo ambayo TAWJA wameyaona ndani ya miaka hiyo 25 tangu kuanzishwa kwake, ni washtakiwa kushindwa kukidhi masharti ya dhamana.
"Pamoja na kwamba dhamana zinakuwa wazi, lakini wahusika wamekuwa wanashindwa kutimiza masharti kwa kukosa baadhi ya mahitaji kama vile wadhamini na vitambulisho, hivyo katika maadhimisho hayo tutalitolea elimu pia," alisema Aisha.
Maadhimisho hayo yatashirikisha wadau mbalimbali wakiwamo majaji na mahakimu wanawake kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, wadau kutoka mashirika ya kimataifa ikiwamo UN Women, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).
Kwa mujibu wa Ripoti ya Takwimu za Msingi Tanzania iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2023, matukio ya ubakaji na ulawiti yanayoripotiwa kwenye vituo vya polisi nchini yameongezeka kutoka 23 kwa siku mwaka 2022 hadi kufikia 31 siku mwaka 2023.
Takwimu hizo pia zinaonesha ulawiti umeongezeka zaidi ya mara mbili mwaka 2023 hadi kufikia matukio 2,488 kulinganishwa na kesi 1,205 zilizoripotiwa mwaka 2020.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED