Wananchi Pangani waomba usafiri wa boti kwenda Unguja Zanzibar

By Hamida Kamchalla , Nipashe
Published at 03:05 PM Dec 23 2024
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa.
Picha:Mpigapicha Wetu
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa.

Baada ya kukumbana na changamoto za muda mrefu za kutumia vyombo visivyo salama kwa usafiri wa majini, wananchi na wafanyabiashara wa Wilaya ya Pangani, mkoani Tanga, wamefunguka na kuwasilisha kilio chao kwa Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa.

Wananchi hao wameiomba Serikali kupeleka huduma ya boti za kisasa itakayorahisisha safari zao kwenda visiwani Zanzibar kwa shughuli mbalimbali, zikiwemo za kibiashara.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Geoffrey Leonard, alieleza kuwa kwa sasa wanatumia fiber boti na majahazi, licha ya Serikali kupiga marufuku usafiri huo kwa sababu si salama. Alifafanua kuwa safari hizo huchukua zaidi ya saa 10 ndani ya maji, jambo linaloongeza hatari kwa abiria na wafanyabiashara.

"Tunaomba tupate boti ya kisasa itakayotuwezesha sisi wa Pangani kufika Unguja kwa haraka. Hivi sasa, watu wanalazimika kutumia njia zisizo rasmi kwa sababu fiber boti zimepigwa marufuku. Wengine hulazimika kusafiri kwa jahazi, safari ambayo huchukua masaa zaidi ya 10 kufika Zanzibar," alisema Leonard.

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, aliposikiliza maombi ya wananchi hao, alisema kuwa Serikali inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wananchi wanafanya shughuli zao katika mazingira salama na rafiki.

"Serikali imeanza maboresho makubwa, ikiwemo uboreshaji wa Bandari ya Pangani na ujenzi wa Barabara ya Kilomita 50 kutoka Tanga hadi Pangani, ambayo itaunganishwa na Bagamoyo. Miradi hii itasaidia kutatua changamoto nyingi za usafirishaji na kuboresha maisha ya wananchi wa maeneo haya," alisema Waziri Mbarawa.

Wananchi wa Pangani sasa wanatarajia Serikali kutekeleza ahadi hizo ili kuboresha huduma za usafiri wa majini na kuimarisha uchumi wa eneo hilo.