TRA Pwani yatoa elimu ya kodi Kibaha

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 04:50 PM Dec 23 2024
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani, Masawa Masatu.
Picha: Julieth Mkireri
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani, Masawa Masatu.

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani, Masawa Masatu, amesema maonyesho ya biashara na uwekezaji yaliyofanyika mjini Kibaha yamekuwa fursa muhimu kwa walipa kodi kupata elimu ya kodi na huduma nyingine muhimu.

Akizungumza wakati wa kufunga maonyesho hayo, Masatu ameeleza kuwa huduma ambazo kwa kawaida hutolewa ofisini zilitolewa moja kwa moja kwa wananchi waliotembelea viwanja vya maonyesho. Hatua hiyo iliwapa wananchi fursa ya kujifunza na kuelewa zaidi masuala yanayohusu kodi, jambo ambalo TRA inaridhika nalo kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi.

"Maonyesho haya ni jukwaa muhimu la kutangaza Mkoa wa Pwani na vilevile kutoa nafasi kwa wananchi kuelewa bidhaa zinazozalishwa katika viwanda vya mkoa huu. Tumefurahia kuona wananchi wengi wakijitokeza na kujifunza kuhusu wajibu wao wa kulipa kodi," amesema Masatu.

Ameongeza kuwa mwitikio wa wananchi kwenye banda la TRA umekuwa wa kuridhisha, na imani yao kubwa elimu iliyotolewa itaongeza uelewa na kuleta mabadiliko chanya katika ulipaji kodi.

Aidha, Masatu amewakumbusha wananchi kuzingatia umuhimu wa kuomba risiti wanaponunua bidhaa, hasa tunapokaribia mwisho wa mwaka. Amesema tabia hiyo inasaidia kuongeza makusanyo ya kodi ambayo yanatumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Maonyesho hayo ya biashara na uwekezaji yamejenga mwamko wa kiuchumi miongoni mwa wakazi wa Mkoa wa Pwani, huku yakihamasisha ushirikiano baina ya wafanyabiashara, wawekezaji, na mamlaka mbalimbali.