SERIKALI kushirikiana na wadau mbalimbali wa masuala ya uchukuzi, ipo katika hatua za kuandaa mapendekezo ya kutunga Sheria ya Bodi ya Uchukuzi, kwa lengo la kuwatambua na kuwasajili wanataaluma hao
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile katika mahafali ya 40 ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), akisema bodi hiyo pia itakuwa na jukumu la kusimamia weledi na maadili ya watalaam wa uchukuzi Tanzania Bara.
Amesema uanzishwaji wa bodi hiyo una lengo la kuhakikisha kazi zote za usafirishaji zinasimamiwa na watu wenye taaluma stahiki.
Akizungumzia kuhusu NIT, Kihenzile amesema serikali itaendelea kukiwezesha chuo hicho, kwa kuboreshea miundombinu ya kufundishia, ili kuhakikisha kinatimiza majukumu yake ya kuandaa wataalam, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu katika sekta ya uchukuzi kwa maendeleo endelevu ya taifa.
Kihenzile alitoa rai kwa wadau mbalimbali wa usafiri na usafirishaji, kuunga mkono jitihada za chuo katika kuwapatia nafasi za mafunzo kwa vitendo wanafunzi na kuendeleza bunifu zinazozalishwa chuoni, ili zitumike kwa maendeleo ya nchi.
Aidha alisema rai kwa wadau na wafaidika wa shughuli za chuo na taasisi za umma na binafsi kuunga mkono jitihada za chuo katika kupata nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi kuendeleza bunifu zinazozalishwa, ili kutumika kwa maendeleo ya nchi.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwamo NIT, ipo katika hatua za kuandaa mapendekezo ya kutunga sheria ya Bodi ya usajili wa wataalam wa uchukuzi lengo likiwa ni kuw tambua, kuwasajili na kusimamka weledi wa maadili ya wataalam wa uchukuzi Tanzania Bara ili kuhakikisha kwamba kazi zote za usafirishaji zinasimamiwa na watu wenye taaluma stahiki,” alisema Naibu Waziri.
Awali, Mkuu wa chuo hicho, Mhandisi Dk. Prosper Mgaya, amesema katika mahafali hayo, wahitimu 4,176 wametunukiwa vyeti katika ngazi mbalimbali kati yao wanaume ni 2,581 na wanawake 1,595.
Akizungumzia changamoto alisema chuo kimekuwa na mikakati ya kukabiliana nazo zikiwamo za miundombinu na upungufu wa rasilimali watu sambamba na ongezeko la udahili wa wanafunzi kwa kuweka mikakati mbalimbali.
Alisema sambamba na mabweni chuo kinajenga ofisi, madarasa na karakana na jumla ya majengo matatu yanajengwa na yanatarajiwa kukamilika Februari 2025, ujenzi huo unafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB), kupitia mradi wa EASTRIP.
Alisema chuo pia kinaanzisha kampasi mpya mkoani Lindi na Kilimanjaro, ili kupunguza msongamano wa wanafunzi katika kampasi ya Dar es Salaam.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED