Polisi yakamata madini ya dhahabu bandia

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 02:41 PM Dec 23 2024
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi
Picha: Marco Maduhu
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi

JESHI la Polisi Mkoa wa Shinyanga, limekamata madini ya dhahabu bandia gramu 250.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amesema hayo leo, akisema ni baada ya msako ambao umefanywa kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 22, 2024.

Amesema katika msako huo, wamekamata jumla ya watu 81 na vingine ni bangi gramu 9,000, mirungi bunda tisa, gongo lita 113, sola panel saba, betri nne za sola, pikipiki 11, kadi tatu za pikipiki, antena nne za ving'amuzi.

Vingine ni redio mbili, baiskeli mbili, mashine moja ya bonanza, kamera moja na mitambo minne ya kutengeneza gongo.

Polisi yakamata madini ya dhahabu bandia
"Katika msako huu tumefanikiwa pia kukamata silaha aina ya gobore kwenye kijiji cha Bugomba A Ushetu wilayani Kahama, mtuhumiwa alikuwa ameibeba kwenye baiskeli na alipoona gari la Polisi alikimbia na kuitelekeza na tuna msaka," amesema Magomi.

Amesema makosa ya usalama barabarani wamekamata makosa 5,376, magari 3,767, bajaji na pikipiki 1609, na wahusika waliwajibishwa na kulipa faini za papo hapo.

Katika hatua nyingine ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu, huku akiwakumbusha wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka.