WATU 11 wamefariki dunia huku wengine 16 wakijeruhiwa katika ajali ya basi la abiria Kampuni ya Capco One lenye namba za usajili T857 DHW lililofeli breki katika mteremko na kurudi nyuma kisha kupinduka.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Brasius Chatanda alisema ajali hiyo ilitokea juzi Desemba 21 saa nane mchana katika Kijiji cha Kabukome, kata ya Nyarubungo, wilayani Biharamulo kwenye eneo la mlima wa kuanzia pori la Kasindaga wakati gari hilo likitoka mkoani Kigoma kuelekea Bukoba, mkoani Kagera.
Kamanda Chatanda alisema chanzo cha ajali hiyo ni mfumo wa breki wa gari hilo kufeli wakati dereva alipolazimisha kusimama katika mlima ili kuruhusu kondakta wa gari hilo kumshusha mtoto ambaye alikuwa amepitilizwa kituo na kumfaulisha katika gari lingine lililokuwa likirudi uelekeo wa kituo alichotakiwa kushuka mtoto huyo.
"Gari lilipotoka Biharamulo kwenda Bukoba lilimpitiliza mtoto mmoja kituo cha kushuka, wazazi wakapiga simu kuwajulisha, hivyo dereva alipokutana na gari aina ya Coaster katika mlima ule, kwa sababu ya haraka akasimamisha gari mlimani na kondakta akashuka na mtoto amwahishe kwenye gari hilo.
"Isivyo bahati, mfumo wa gari upande wa breki na gia vyote vikagoma, gari likaanza kurudi nyuma, likamshinda dereva, likatoka nje ya barabara na kubinuka na kusababisha vifo na majeruhi. Miili yote ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Biharamulo huku watu 16 wakijeruhiwa na baadhi yao wanaendelea vizuri hospitalini hapo," alisema Kamanda Chatanda.
Akithibitisha kupokea miili na majeruhi hao, Mganga Mkuu wa Hospitali Teule ya Biharamulo, Gresmus Sebuyoya alisema walipokea miili ya watu 11. Kati yao, wanaume ni wanne, wanawake watano, mtoto wa kiume mmoja na wa kike mmoja na kuwa miili yote imehifadhiwa hospitalini huko.
Kuhusu majeruhi, alisema 26 tayari wameruhusu huku wengine 16 wakiendelea na matibabu na uangalizi wa karibu.
Dk. Gresmus alisema waliobaki hospitalini huko kwa uangalizi na matibabu ni pamoja na watoto wanne ambao wanaendelea vizuri, wanaume sita pamoja na wanawake sita.
Akizungumza baada ya kutembelea majeruhi hospitalini, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, alisema wizara imeanza kufanyia kazi maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya marekebisho ya kuwa na mfumo wa leseni.
Alisema katika mfumo huo wa leseni za udereva, utakuwa ukiwapunguzia alama madereva wanaofanya makosa yenye kuhatarisha usalama barabarani ambazo zitasaidia kuwafungia leseni.
Alitoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wote walioguswa na ajali hiyo na kutoa wito kwa watanzania kuendelea kuwaombea majeruhi wapone haraka.
"Nitumie nafasi hii kuombea roho za marehemu ambao tumewapoteza katika ajali ambayo imetokea hapa Biharamulo, tumepoteza ndugu zetu 11, wametangulia mbele za haki," alisema Waziri Bashungwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED